Thursday, 12 March 2015

Kura ya maoni yaahirisha Baraza la Wawakilishi.



Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kutoka Chama cha Wananchi (CUF) jana walizua vurugu katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi na kumlazimisha Spika wa Baraza hilo, Pandu Ameri Kificho, kuahirisha kikao hicho.


Fujo hizo zilitokea kabla ya kuwasilishwa kwa sheria ya kura ya maoni namba 11 ya mwaka 2013 ya Jamuhuri ya Muungano kwa mujibu wa kifungu 132(2) cha Katiba ya Zanzibar.

Wabunge wa CUF walikuwa awanapinga kuwasilishwa kwa sheria hiyo na baada ya vurugu hizo kuendelea takribani kwa zaidi ya nusu saa huku Spika Kificho akihamasisha hali ya utulivu barazani, lakini lishindikana na kuwataka wasaidizi wake kunyanyua siwa na kuanza kutoka huku wajumbe wengine wakicheza na kuendelea kushangilia.
Wakati wajumbe hao wa CUF wakishangilia na kuimba kwamba CCM ni madalali wa Zanzibar, wajumbe wa CCM nao walisimama na kuimba CCM, CCM, CCM hivyo hali iliyoligeuza Baraza kugeuka kama ni chumba cha studio cha kurekodi muziki.

Kabla ya kuanza kwa vurugu hizo, mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, alisema kuwa hawakubaliani na sheria hiyo kwani Zanzibar ina sauti yake, hivyo hawezi kutumia kanuni ya Jamuhuri ya Muungano kwani kufanya hivyo ni sawa na kuwa dalali kwa Zanzibar.

“Nasema sheria hii sisi hatuikubali kwani sisi hatutaki kuwa madalali wa Zanzibar, sheria hii tukiikubali tutakuwa ni madalali,” alisema Jussa.

Baada ya kauli hiyo ya Jussa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Raisi (Utawala Bora), Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini, alilazimika kusimama na kumtaka Jussa kufuta kauli yake ya kuwahusisha Wajumbe wa Barala kuwa ni madalali wa nchi na kumtaka kuomba radhi. Kutokana na hali hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Said Hassan Said, alilazimika kusimama na kueleza kuwa hoja hiyo haina msingi na ilitakiwa mawazo kama hayo kujitokeza wakati wa utungaji wa sheria yenyewe hasa kwa kuzingatia kuwa Baraza la Wawakilishi kwa mujibu ibara ya 66(1) C ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano lina wajumbe watano wanaingia katika Bunge la Jamhuri ya Muungano.

“Hayo yote wanayoyasema yalikuwa yaelezwe wakati wa kutengenezwa sheria katika Bunge la Jamhuri ambalo lina wajumbe watano kutoka Baraza la Wawakilishi wanaoliwakilisha baraza hili, sasa leo wasisimame hapa na kusema hawataki udalali,” alisema Mwanasheria Mkuu.

Alisema utaratibu unaotumika wa kuwasilisha hati mezani upo kwa mujibu wa kanuni na upande wa Serikali umezingatia taratibu zote na kutaka Baraza liendelee na utekelezaji wa majukumu yake ya kuwasilisha sheria ya kura za maoni.

Hata hivyo, Spika Kificho alisema pamoja na kujitokeza vurugu hizo, kazi ya kuridhia sheria hiyo imeshafanyika kwa vile ilikuwa ikitakiwa ni kusomwa hati ya kuwasilisha mezani hatua ambayo tayari ilifanyika na haihitaji kujadiliwa na kupigiwa kura.


CHANZO: NIPASHE