Sunday, 24 May 2015

LEMA:POLISI WAKITUMIKA KISIASA NA CCM, UKAWA TUTAJILINDA WENYEWE

Kambi ya upinzani imesema italazimika kujilinda katika mikutano ya kampeni za uchaguzi mkuu, endapo polisi wataendelea kutumiwa kisiasa na kuwaacha green guards wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kufanya fujo kwenye mikutano yao.

Msemaji mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema, alisema hayo alipokuwa akisoma hotuba ya kambi hiyo kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2015/16.

Alisema vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Watanzania (Ukawa), vinatoa tahadhari kwa CCM, endapo wamepanga njama zozote zile kuhujumu vyama vyao katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, mwaka huu.

“Njama hizo zitadhibitiwa ipasavyo kwa sababu upinzani wa sasa hivi una nguvu kuliko wakati mwingine wowote,” alisema.

Alisema kwa kuwa taifa linaelekea kwenye uchanguzi mkuu, na kwa kuwa kipindi cha uchaguzi ni kipindi ambacho amani ya nchi inatakiwa kulindwa kwa nguvu zaidi kuliko vipindi vingine, upinzani unatoa angalizo kuhusu kutochezea haki za mwananchi kujiandikisha kuwa mpiga kura na kutofanya mzaha na uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi.

UCHOCHEZI WA KIDINI NA KIKABILA Lema alisema tatizo la udini na ukabila limeendelea kuwa hatari kwa ustawi wa amani ya nchi na hilo ni janga kubwa ambalo linaratibiwa na CCM na washirika wake kwa maslahi ya kisiasa.

“Wakati uchochezi huu wa kidini na kikabila ukifanyika, Usalama wa Taifa wanajua, polisi wanajua lakini hawachukui hatua yoyote.
“Nadhani wanafikiri kwamba ni mkakati mzuri wa ushindi kwa CCM lakini kumbe ni mkakati unaohatarisha hali ya usalama na amani nchini,” alisema.

TUME YA UCHUNGUZI WA KIMAHAKAMA Alisema kwa kipindi chote cha miaka 10 ya serikali ya awamu ya nne, kambi ya upinzani imepigia kelele na kulaani mauaji ya raia wasio na hatia yanayofanywa na vyombo vya dola hususan, polisi.

Alisema kambi hiyo imeikumbusha serikali kuunda Tume ya Uchunguzi wa Kimahakama kuchunguza vifo hivyo kwa mujibu wa sheria ya kuchunguza vifo vyenye utata.

VITAMBULISHO VYA TAIFA Alisema inasikitisha kuona tangu mchakato huo uanze, serikali haitoi mrejesho wa namna zoezi hilo linavyoendelea.

“Ni wananchi wangapi wameshapata vitambulisho hivyo, ni lini kila raia wa Tanzania atakuwa amepatiwa kitambulisho chake cha taifa, na ni fedha kiasi gani zimetumika hasi sasa katika mchakato huo,” alisema.

MAZINGIRA NA AFYA ZA MAHABUSU NA WAFUNGWA Alisema serikali imeshindwa kupunguza msongamano wa mahabusu na wafungwa magerezani kwa kubuni adhabu mbadala za nje kwa makosa madogo madogo badala ya vifungo.

Alisema serikali hii imeshindwa pia kufanya upelelezi wa kesi zinazowakabili watubumiwa wa makosa mbalimbali kwa wakati na hivyo kusababisha msongamano wa mahabusu magerezani.

Kuhusu afya alisema wanaitaka serikali kuchukua hatua za haraka kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu magerezani sambamba na kuboresha lishe na huduma za afya kwa wafungwa na mahabusu.

CHANZO: NIPASHE