Shirika la fedha duniani
limeonya jumuiya ya Afrika Mashariki dhidi ya kuharakisha mpango wake wa kutaka
kuwa na sarafu moja.Mataifa ya jumuiya hiyo yalIanzisha mkakati wao wa kutaka
kubuni sarafu moja inayoweza kutumika katika nchi wanachama ili kurahisisha
biashara katika kanda hiyo.
Mataifa tano wanchama wa jumuiya hiyo mwishoni mwa
mwezi Novemba mwaka jana, yalitia saini mkataba wa kuanza mkakati wa kutafuta
sarafu moja katika kipindi cha miaka kumi ijayo , mpango wanaotumai utapanua
biashara katika kanda hiyo nzima.
Mpango huu utashuhudia
nchi hizo zikiwianisha sera zao za kifedha na kuchumi na kuweza kubuni benki
kuu moja.
Kenya, Uganda, Tanzania na
Rwanda tayari husoma bajeti zao kila mwezi Juni.
Ushauri huu kutoka kwa
shirika la fedha duniani, unakuja wakati kanda ya Ulaya ingali inakumbwa na
matatizo ya kiuchumi kutokana na viwango vikubwa vya madeni yao huku mataifa
wanachama wakikabiliwa na ukosefu wa ajira.
Mkuu wa shirika hilo
ambalo yuko ziarani Kenya, Christine Lagarde amesema kuwa kuwianisha sera za
kifedha ni wazo zuri lakini pia ni changamoto kubwa.
Bi Lagarde alisema itakuwa
muhimu kwa Kenya kutoa funzo kutoka katika mataifa ya Euro ambayo yanatumia
sarafu moja na kusoma aina ya changamoto zinazokabiliwa nazo.
Ziara ya Bi Lagarde nchini
Kenya ni kama jambo la kawaida kwa shirika la fedha duniani kuhakikisha kuna
uthabiti wa kiuchumi katika sehemu mbali mbali duniani.
Kenya ni nchi ya pili kwa
ukubwa kwa uwekezaji katika kanda ya Afrika Mashariki.
Kuweka wazi soko la pamoja
la biashara kwa mataifa wanachama wa mataifa ya Afrika Mashariki itakolesha
biashara na kuinua maisha ya watu wa kipato cha kadri ambao wanastawisha zaidi
uchumi.