Monday 18 May 2015

Rais Nkurunziza atimua na kupangua Baraza la Mawaziri

Siku sita baada ya jaribio la mapinduzi kutofanikiwa, rais wa Burundi Pierre Nkurunziza amefanya mabadiliko katika serikali yake Jumatatu wiki hii.

Mawaziri watatu ikiwa ni pamoja na Waziri wa Ulinzi, Jenerali Pontien Gaciyubwenge, Waziri wa Mambo ya Nje, Laurennt Kavakure pamoja na Waziri wa Biashara, wamefutwa kazi.

Alain Nyamitwe, kaka wa Willy Nyamitwe, Mshauri Mkuu wa rais Nkurunziza katika masuala ya mawasiliano, ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje. Alain Nyamitwe amechukua nafasi ya Laurent Kavakure.
Emmanuel Ntahomvukiye , ambaye ni raia wa kawaida, ameteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi, akichukua nafasi ya Jenerali Pontien Gaciyubwenge. Hii ni mara ya kwanza tangu Burundi ipate uhuru wake kwa raia wa kawaida kuteuliwa kuchukua nafasi hiyo.

Bi Irina Inantore ameteuliwa kuwa Waziri wa Biashara.

Sababu za mabadiliko hayo hazijafahamishwa, lakini inasemekana kuwa Laurent Kavakure amefutwa kazi baada ya kushindwa kushawishi Jumuiya ya Kimataifa kuhusu muhula wa tatu wa rais Pierre Nkurunziza.

Inasadikiwa pia kuwa huenda Jenerali Pontien Gaciyubwenge amefutwa kazi kutokana na kushindwa kumkamata Jenerali Godefroid Niyombare, ambaye alitangaza hivi karibuni kuuwangusha utawala wa Pierre Nkurunziza.

Mkuu wa Majeshi Jenerali Prime Niyongabo amepewa majukumu makubwa ya kusimamia na kuliongoza jeshi.

Wakati hayo yakijiri, maandamano yameendelea katika wilaya mbalimbali za jiji la Bujumbura. Pia, wameonekana wanajeshi wakiunga mkono waandamanaji, huku wengine wakiwaonya kusitisha maandamano hayo