MAWAZIRI wa Afrika Mashariki kutoka nchi tano za Jumuiya ya
Afrika Mashariki (EAC), walikutana jana kwa saa 1:08 asubuhi jijini hapa
kujadili hali ya uchaguzi nchini Burundi kutokana na maazimio matatu.
Miongoni mwa maazimio hayo ni kuitaka
Tume ya Uangalizi ya Uchaguzi wa Burundi kutoka nchi za EAC, inayoongozwa na
Jaji Joseph Warioba kuendelea na kazi hiyo nchini humo mara moja.
Aidha, imeazimiwa kuwa, Mwenyekiti wa
Baraza la Mawaziri wa EAC, Dk Harrison Mwakyembe na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya
EAC, Dk Richard Sezibera kutembelea Burundi mapema iwezekanavyo kwa lengo la
kujionea hali halisi katika nchi hiyo.
Kikao hicho cha dharura kilichofanyika
makao makuu ya EAC jijini hapa kuanzia saa 6:12 mchana na kumalizika saa 7:24
mchana huo kikiwa chini ya uenyekiti wa Dk Mwakyembe, kilihudhuriwa na karibu
mawaziri wote wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, isipokuwa,
Valentine Rugaine wa Rwanda ambaye haikuelezwa sababu za kushindwa kushiriki.
Dk Sezibera alizungumza na wanahabari
na kusema moja ya mambo yaliyojadiliwa katika kikao hicho ni pamoja na kupokea
taarifa ya kikao cha wanasheria wakuu wa nchi za EAC, kilichofanyika mwishoni
mwa wiki jijini hapa. “Baraza la mawaziri limepokea taarifa ya kikao cha
wanasheria wakuu wa nchi za EAC kilichokuwa na lengo la kujadili hali ya
Burundi.
“Taarifa hii iliyowasilishwa
itakabidhiwa kwa wakuu wa nchi za EAC katika mkutano wa makuu hao unaotarajiwa
kufanyika hivi karibuni,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk Sezibera baraza hilo
la mawaziri, liliazimia mambo makuu matatu, ikiwa ni pamoja na Tume ya Jaji
Warioba kuendelea na kazi hiyo nchini Burundi, Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri
wa EAC na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo kutembelea Burundi, huku mawaziri wa EAC
wakipewa jukumu la kutembelea kambi za wakimbizi zilizopo Rwanda na Tanzania
kwa lengo la kujionea hali halisi ya maisha ya wakimbizi katika kambi zote
zilizopo katika nchi hizo.
Awali, Waziri anayeshughulikia Afrika
Mashariki kutoka Burundi, Leontine Nzeyimana aliwataka wananchi wa Burundi kuwa
watulivu katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu.
Aidha, aliwataka wananchi hao kutambua
kuwa Burundi ni mali yao na hawana nchi nyingine, hivyo ni vyema wakawa na
subira kwa kuwa uchaguzi upo pale pale.
Kikao hicho cha dharura ni mwendelezo
wa vikao vya kutafuta suluhu ya machafuko ya kisiasa, yanayoonekana kuinyemelea
Burundi hasa baada ya Rais Pierre Nkurunziza kutangaza kuwania urais kwa awamu
ya tatu katika uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
Uamuzi huo unapingwa na makundi kadhaa
na wiki iliyopita Nkurunziza alinusurika kupinduliwa na mahasimu wake.