Tuesday, 26 May 2015

BAADA YA KUSAINI MKATABA NA YANGA FC, MWINYI HAJI AFUNGUKA HAYA..

YANGA SC imekamilisha usajili wa mlinzi wa kushoto kutoka Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo Zanzibar (KMKM), Mwinyi Hajji ili kumpa changamoto Oscar Joshua na Edward Charles wanaocheza nafasi hiyo.

Mwinyi, mchezaji wa Taifa Stars, jana makao makuu ya klabu hiyo, Jangwani, Kariakoo, Dar es salaam alisaini mkataba wa miaka miwili kuwatumikia mabingwa hao wa Tanzania bara.
Tumefanya mahojiano maalumu na Mwinyi kujua baadhi ya mambo kutoka kwake;

Swali: Zipo timu nyingi Tanzania bara, lakini umeamua kusaini Yanga, kitu gani kimekuvutia?

Mwinyi: Nilikuwa na ndoto tangu zamani kwenda Yanga na sasa nimesaini mkataba wa miaka miwili. Hakika ndoto zangu zimetimia!, nitaichezea Yanga.

Swali: Wachezaji wengi wa Tanzania hawapendi kutaja kiwango cha fedha walichosajiliwa, vipi wewe unaweza kutuambia umesaini kwa shilingi ngapi?

Mwinyi: Hiyo ni siri yetu yaani mimi na klabu!, si unajua tena katika maisha! binadamu mara hivi, mara vile! Inabidi ibaki kuwa siri yangu na klabu tu, baaaasi!

Swali: Yanga ni klabu kongwe na mabingwa mara nyingi zaidi wa Tanzania bara, familia yako imepokeaji taarifa za wewe kusajiliwa na klabu hii?

Mwinyi: Wamenipokea kwa mikono miwili na heshimu zote, unajua maombi yao ndio yamenifikisha hapa nilipo.

Swali: Baada ya kusaini umeendelea kuvaa vitu vyenye rangi ya Yanga, tunaona kofia, fulani, saa ya mkononi vyote ni Yanga, hayo ni mapenzi  baada ya kusajiliwa?

Mwinyi: Sio mapenzi baada ya kusajiliwa, tangu zamani naipenda Yanga, hata ukinichinja! damu itakayotoka ni rangi ya Yanga. kwasasa nimeingia katika jukumu la kuitumikia klabu hii.

Swali: Ni ngumu kujua furaha aliyonayo mwanadamu moyoni mwake baada ya kufanikiwa jambo fulani, vipi wewe umejisikiaje kusajiliwa Yanga?

Mwinyi: Nimejisikia furaha sana, maisha yangu yanaanza kufunguka-funguka. Jua tu nimefurahi sana kusajiliwa Yanga.

Swali: Ilikuwa rahisi kufikia mafanikio ya kusajiliwa Yanga?

Mwinyi: Haikuwa rahisi, lazima ujitume. Kujituma kwangu ndio kumenifanya nionekane na kusajiliwa Yanga.

Swali: Vitu gani vya pekee vimesababisha uonekane wewe tu na si mchezaji mwingine wa Zanzibar?

Swali: Kwanza niseme ni heshima, halafu pili kiwango na kujituma kwangu. Yanga wameniona kutokana na juhudi zangu uwanjani.

Swali: Unaiambia nini klabu yako ya KMKM?

Mwinyi: Hakika nawashukuru sana kwa kunitunza kutoka mwaka jana mpaka hivi  leo (jana) nasaini Yanga, dolegumba hili hapa! nimesaini Yanga. KMKM pia wamenipa heshima, naipenda vilevile!

Swali: Hukuzaliwa na kuanza timu ya Chuoni, halafu ukaenda KMKM na sasa Yanga, tuambie hapo mwanzo umewahi kuchezea timu gani?

Mwinyi: Nilianza kucheza timu yangu ya Mapunda Tottenham ya daraja la pili, kutoka hapo nikaenda Maji Maji, baadaye nikajiunga na Chuoni, halafu KMKM na sasa Yanga.

Swali: Changamoto gani umekumbana nazo mpaka kufikia Yanga?

Mwinyi: Zipo changamoto nyingi kama vile kutupiwa lawama, kukatishwa tamaa, lakini nikasema sikati tamaa, nitajitahidi ili namimi nije kuonekana katika nchi hii.

Swali: Mwaka jana katika kutimiza miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ulikuwa mchezaji bora wa kombe la Mapinduzi, unadhani hii pia imekuongezea sifa ya kusajiliwa Yanga?

Mwinyi: Ndiyo! Imeniongezea sifa kwasababu mimi ndiye nilikuwa mchezaji bora, nilionesha kiwango japokuwa tulitolewa robo fainali na Simba tukifungwa 2-0 uwanja wa Chuoni.

Swali:  Una uwezo mzuri wa kupiga mipira ya adhabu ‘Free kick’ na kufunga, unawaahidi wanayanga kuwa utaendeleza hilo?

Mwinyi: Nitazidisha kiwango changu kuliko nyuma, nitawafurahisha Wanayanga, tutatunza heshima ya kutetea ubingwa wetu. Tushirikiane na kufanya kazi nzuri, kwa nguvu ya pamoja tutafanikiwa.


CREDIT:Shafiihdauda.com