OSCAR Joshua kwasasa ndiye
mlinzi wa kushoto chaguo la kwanza katika klabu ya Yanga na mbadala wake ni
Edward Charles.
Beki wa kushoto wa yanga,Oscar Joshua
Joshua hana kasi, hawezi kusaidia timu kushambulia, hivyo Yanga wameamua
kutafuta mlinzi wa pembeni mwenye uwezo wa kulinda, kushambulia na kufunga
magoli. Ni nani huyo? Jibu ni Mwinyi Hajji kutoka KMKM.
Mwinyi alisainishwa jana mkataba wa miaka miwili kuitumikia Yanga na ndipo mtandao huu umeamua kumtafuta katibu mkuu wa Yanga, Dr. Jonas Tiboroa kutaka kujua sababu za kumchukua nyota huyo.
Mwnyi Haji akisaini mkataba na Yanga FC
Dr. Tiboroa anajibu: “Kwa muda mrefu hatujaweza kuwa na mchezaji namba 3 mwenye uwezo kama wa Mwinyi. Sio uwezo wa kulinda tu bali kuweza kushambulia na kufunga magoli”.
“ Kumbuka huyu kijana licha ya kuwa mlinzi ndiye mfungaji bora wa KMKM. Tuliona ana faida kwenye timu yetu na kuweza kumsajili”.
“Tumetumia muda mwingi sana kumchambua na kumuangalia, tumefanya kazi hiyo kwa takribani miezi mitano, sasa tukaona ni wakati mzuri wa kumsajili”.
Swali: Usajili wa Mwinyi unatoa ishara gani kwa Oscar Joshua?
Dr. Tiboroa: Ni kumsukuma Oscar Joshua aweze kuwa mzuri zaidi ya sasa, narudia tena, timu yoyote iliyopo kwenye kiwango alichopo Yanga inahitaji kuwa na wachezaji zaidi ya wawili kwenye nafasi moja, tena wenye kiwango kizuri, wanaoweza kucheza nafasi zaidi ya moja. Lengo letu ni kuendelea kuimarisha timu, iwe na nguvu zaidi ya mwaka mwaka jana.
Swali: Yanga imekamilisha usajili wa Deus Kaseke, Benedictor Tinocco na Mwinyi Hajji. Wachezaji hawa ni vijana wadogo, je, umefika wakati wa Yanga kuamini vijana?
Dr. Tiboroa: Kilichosababisha kusajili vijana ni falsafa ya timu na namna inavyocheza mpira. Inahitaji kuwa na wachezaji wenye kasi, hupati mwendo kasi kutoka kwa mtu mwenye umri mkubwa, ndio maana tunachukua vijana.
Kumbuka vijana
kwenye mpira unaweza kumwambia shika waya wa umeme, akashika kwasababu ana nia
ya kufanya kitu fulani. Yanga kwasasa tunachukua vijana, lakini sio vijana tu,
tunataka vijana wapambanaji watakaoifanya Yanga ishinde.