KAMATI
ya Ukweli na Maridhiano ya Chama cha Tanzania Labour (TLP), imetangaza kumvua
uanachama Mwenyekiti wa chama hicho, Agustino Mrema.
Akizungumza
jana, jijini Dar es Salaam na vyombo vya habari, Mwenyekiti wa Kamati hiyo,
Joram Kinanda alisema kuwa kamati hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kupitia kwa
kina malalamiko yaliyokuwa yakimuhusu Mrema, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo.
Mwenyekiti
huyo alisema kuwa mbali na Mrema wengine waliovuliwa uanachama ni Hamisi
Mkadamu, Antoni Mapunda, Nancy Mrikaria, Dominata Rwechungura, Maxmilian Lymo,
Richad Lyimo, Hamisi Mkumba na Stanley Temba.
Kinanda
alisema kuwa wanachama hao wamevuliwa uanachama kwa mujibu wa katiba ya chama
hicho, toleo la 2005 Ibara ya 9.9 (c) na 2009 ibara 9.5(c).
Kinanda
alisema kuwa maazimio hayo yamepelekwa katika ofisi ya msajili wa vyama vya
siasa kwa taratibu za kisheria pamoja na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kwa
upande wake Msajili Msaidizi wa Vyama Vya Siasa nchini, Sisty Nyahoza, alipotafutwa
ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, alisema kamati hiyo haitambuliki kisheria.
“Kamati
hiyo haitambuliki kisheria, na hata Mrema mwenyewe amekuwa akipinga TLP kuwa na
kamati ya aina hiyo na hata viongozi wake hawatambuliki, ” alisema
CHANZO:
MTANZANIA