Saturday 11 April 2015

DANI ALVES AKATAA OFA YA KUSAINI MKATABA MPYA NA BARCELONA


Beki wa pembeni kutoka nchini Brazil, Daniel Alves da Silva na club ya Barcelona, amekataa ofa ya kuongezewa mkataba na klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao na wakala wake tayari amethibitisha hilo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na wakala wa beki huyo mwenye umri wa miaka 31, Dinorah Santa Ana, imeelezwa kwamba uongozi wa FC Barcelona huenda ukaanza mazungumzo ya kumsainisha mkataba mpya Dani Alves wakati wowote kabla ya mwishoni mwa msimu huu.

Dinorah Santa Ana ambaye alikuwa mke wa Dani Alves ameongeza kwamba suala hilo kwake analipa nafasi kubwa kutokana na kuamini kwamba kuna uwezekano wa pande hizo mbili zikafikia maamuzi na kusaini mkataba mpya.

Gazeti la Mundo Deportivo, limeripoti kwamba Santa Ana alikuwa na kikao kilichotumia muda wa saa mbili dhidi ya viongozi wa FC Barcelona usiku wa kuamkia jana kwa lengo la kufahamu mustakabali wa mchezaji wake kutokana na nafasi aliyo nayo hivi sasa huko Camp Nou.

Beki huyo wa zamani wa Sevilla amekuwa akihusishwa kuhamia Manchester United,Manchester City zote za England pamoja na PSG ya Ufaransa.