Katika siku za hivi karibuni kumeibuka tabia ya
baadhi ya watu wachache wasiofahamika kutunga na kusambaza ujumbe kupitia simu
za mikononi na mitandao mbalimbali ya kijamii wenye lengo la kuwatia hofu
wananchi, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Aidha, watu hao wanaosambaza
taarifa hizo wanajifanya kwamba taarifa hizo zimetoka kwenye taasisi za
kimataifa na taasisi zingine zinazoaminika jambo ambalo siyo kweli.
Jeshi la Polisi nchini linawataka wote wenye tabia
hiyo kuacha mara moja na badala yake, endapo mtu yeyote anayo taarifa ya
uhalifu wa aina yoyote ama kikundi chochote cha uhalifu atoe taarifa hiyo
katika kituo chochote cha Polisi au kupitia simu za makamanda wa polisi wa
mikoa ama vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili taarifa hizo ziweze
kufanyiwa kazi haraka.
Aidha, Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa
taarifa zote zinazopokelewa ili kuhakikisha kwamba usalama wa raia na mali zao
unaendelea kuimarika. Hata hivyo, Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua
mtu yeyote atakayebainika kusambaza ujumbe wenye mlengo wa upotoshaji,
uchochezi ama kuwatia hofu wananchi.
Imetolewa na:-
Advera Bulimba -SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.