Tuesday, 17 March 2015

Waraka wa wazi kwa Waheshimiwa Tundu Lissu, Mdee na Wenje Kufuatia Kufukuzwa Kwa Zitto Chadema




Mwishoni mwa juma lililopita uliibuka mjadala juu ya kauli za baadhi ya viongozi wa juu wa CHADEMA kuhusiana na kufutwa uanachama kwa Mbunge wa Kaskazini Mhe.Zitto Kabwe.

Mjadala mkubwa ulikua juu ya kauli za wabunge watatu wa CHADEMA ambao ni Mhe.Tundu Lissu, Halima Mdee na Ezekia Wenje.


Mjadala ulianza baada ya Lissu kueleza msimamo wa Katiba juu ya hatma ya mwanachama aliyefungua kesi mahakamani dhidi ya chama na akashindwa. Je nini kinatokea?

KWANINI LISSU ALIKUA SAHIHI.

Lissu alieleza msimamo wa Katiba. Alichokisema Lissu si mawazo yake. Ingekuwa mawazo yake bila shaka hata mimi ningempinga, lakini kwa kuwa ni msimamo wa katiba huwezi kupinga unless uombe Constitutional amendment kwa taratibu zilizowekwa.

So hata kama angesema mtu mwingine ambaye si Lissu angesema kauli ileile aliyoisema Lissu kwamba "ukifungua kesi mahakamani dhidi ya chama na ukashindwa unakuwa umejifukuzisha uanachama mwenyewe".

Kwa hiyo sio mawazo ya Lissu, ni msimamo wa katiba. Yani hata angesema Mbowe, Dr.Slaa, Mnyika au mwingine yeyote angesema vilevile alivyosema Lissu.

Wapo wanaohoji kwanini Lissu aseme na sio Mbowe ambaye ndiye mwenyekiti? Jibu lake ni kuwa masuala ya kisheria ndani ya chama yanaweza kusemewa na mwanasheria wa chama. Na wanasheria wa chama ni pamoja na Lissu, John Mallya, Mabere Marando na wengineo.

Sasa nashangaa wanaohoji uhalali wa Lissu kuongelea msimamo wa katiba ambalo ni jambo la kisheria. Mmesahau kuwa Lissu ni mwanasheria wa Chama? Sasa kama mnajua Lissu ni mwanasheria wa chama mnashangaa nini anapotoa ufafanuzi wa kisheria? Au mlitaka mambo ya sheria ayaongelee mlinzi wa Dr.Slaa?

Wengine wamehoji kwanini baada ya ile hukumu hakikukaa kikao kikaafikiana kumfukuza Zitto badala ya Lissu tu kusema. Hawa ni wale ambao hawajui hata wanachozungumza. Either ni watu wa vyama vingine so hawaijui katiba ya CHADEMA au ni wapenzi wa chadema lakini hawapendi kusoma.

Sasa kwa kuwasaidia ngoja niwaambie hivi. KATIBA ya CHADEMA ya mwaka 2006 inasema mwanachama yeyote atakayekipeleka chama mahakamani na akashindwa anakua amejifukuzisha uanachama mwenyewe. Hii ina maana kuwa baada tu ya hukumu kutoka automatically yeye sio mwanachama tena.

So bila haya Lissu kuongea lolote, Zitto alishajua yeye sio mwanachama tena. Thats legal stand.

Katiba haikusema hukumu ikishatoka kamati kuu ikae itoe tamko NO. Katiba inasema hukumu ikitoka kama umeshindwa kesi fungasha virago katafute chama kingine.

Kwa hiyo hata kama chama kisingesema lolote. Yani Lissu angekaa kimya na viongozi wengine wote wakakaa kimya, Zitto angeondoka tu.. maana hakuna namna nyingine. Na ungemfuata Zitto umuulize akaamua kuwa honesty angekuambia wazi kuwa kikatiba amejifukuza uanachama mwenyewe.

Kwa hiyo kama kuna tatizo, basi tatizo halipo kwa Lissu au Mallya au mwanasheria yeyote wa Chadema. Kama kuna tatizo basi Tatizo lipo kwenye Katiba ya chama.

Na ikumbukwe wakati kipengele hicho cha katiba kinaundwa mwaka 2006 Tundu Lissu hakuwa hata mwanachama wa CHADEMA (alikua Nccr Mageuzi), so huwezi kuhoji legitimacy yake kwenye hicho kipengele.

Labda ambaye anaweza kuhojiwa kwanini kipengele hicho kiliwekwa na akatoa maelezo mazuri ni Mhe.Zitto Kabwe ambaye wakati marekebisho ya katiba yanafanyika mwaka 2006 yeye alikuwa mjumbe wa Kamati Kuu.

Kwa hiyo yeye ndiye anayeweza kutupa logic ya hicho kipengele. Walikiweka ili iweje? Walimlenga nani? Kama alishiriki kuweka kipengele hicho mbona analalamika kinapotumika kwake? Alitaka kitumike kwa nani?

Ikumbukwe sheria ni msumeno hukata huku na huku. Unapotunga sheria yoyote jiulize hii sheria ikitumika kwangu nitajisikiaje? Sio unatunga then ikikurudia unahisi umeonewa.

Viongozi wengi wa kiafrika wanapotunga sheria kandamizi (Draconian Laws) hudhani ni kwa ajili ya tabaka la chini tu na sio kwa ajili yao. Siku zikiwageuka wanaanza kutafuta mchawi. Katika hili Zitto hapaswi kulalamika kabisa kuhusu kifungu cha katiba kinachomvua uanachwma maana alishiriki kukitunga mwaka 2006.

KWANINI MDEE ANAPASWA KUJIUZULU.

Halima Mdee alitweet kile alichokiita "mawazo yake" kuwa yeye anaamini Zitto bado ni mwanachama wa CHADEMA.

Pamoja na kuwa ni mawazo yake lakini amekosea kwa kuwa yeye kama kiongozi mkuu ndani ya CHADEMA hakupaswa kukosoa chama chake mitandaoni. Hii ni kwa sababu anazo platform nyingi za kukikosoa chama zaidi ya mitandaoni kama alivyofanya.

Yeye ni mjumbe wa Kamati kuu angeweza kuyasema huko. Yeye ni M/kiti wa BAWACHA angeweza kuyasema huko, yeye ni mjumbe wa Baraza kuu la chama angeweza kuyasema huko. Yeye ni mjumbe wa mkutano mkuu, angeweza kuyasemea huko.

Kwa kifupi Mdee alikua na fursa nyingi za kusemea hayo mawazo yake badala ya kusemea mitandaoni. Huku mitandaoni ni kwa wale wasio na fursa ya kuwasilisha mawazo yao moja kwa moja kama ilivyo kwa Mdee. So katika hili amekosea.

Pili, Mdee anajua kuwa maamuzi ya Zitto kuvuliwa uanachama ni ya Katiba si ya mtu mmoja. Si ya Lissu wala Mbowe. Ni maamuzi ya Katiba. Na Katiba hiyo Mdee alishiriki kuitunga mwaka 2006 akiwa Mbunge viti maalum na mjumbe wa kamati kuu. Leo anawezaje kupinga kitu kilekile alichoshiriki kukitunga? Huu ni wendawazimu.!

Lakini pia Mdee anajua kuwa hata kama ameona kasoro kwenye suala hili, ni kasoro za kikatiba sio za Lissu au Mbowe. Hivyo basi mahali pazuri pa kurekebisha kasoro hizo ni kwenye vikao vya chama si mtandaoni kama alivyofanya. Maana hata akitweet kila siku kuwa anamtambua ZZK kuwa mwanachama, bado Katiba iko palepale kuwa haimtambui.

Nne, Mdee ni kiongozi wa Baraza la Wanawake na alipochaguliwa alikula kiapo cha kuilinda Katiba ya chama. Katiba aliyoapa kuilinda ndiyo hiyohiyo inayosema "mwanachama akikipeleka chama mahakamani akashindwa kesi amejivua uanachama wake mwenyewe."

Sasa mbona Mdee anapingana na katiba aliyoapa kuitetea na kuilinda? Hii ni ajabu. Au alipoapa hakujua ndani kuna nini? Aliapa kuilinda katiba asiyoijua? Lakini ataachaje kuijua na alishiriki kuitunga mwaka 2006? This is paradox.!

Katika hili Mdee kadhalilisha nafasi yake kama Mwenyekiti wa Baraza la wanawake na mimi nashauri AJIUZULU ili kuonesha dhana ya uwajibikaji. Ni lazima viongozi wajifunze kuwajibika kwa kauli zao.

Hatuwezi kila siku kupigia kelele mawaziri wa serikali ya CCM wawajibike wakati sisi wenyewe dhana ya uwajibikaji inatushinda. Kipimo kilekile tunachowapimia CCM nasi tujipimie vivyo hivyo. Mdee achia ngazi maana umeikana Katiba uliyoapa kuitetea.

KWANINI WENJE YUPO SAHIHI,

Ujumbe uliosambaa ukionesha ni wa Ezekiah Wenje akichat na wabunge wenzie kwenye group la Whatsapp juu ya sakata la Zitto nao umeibua mjadala mkubwa kwenye jamii. Wengine wakisema ni wake wengine wakidai ni photoshop. Na wale waliosema ni wake nao wakagawanyika. Wengine wakasema alikua sahihi huku wengine wakiponda kuwa amekosea.

Ili kujiridhisha kabla sijacomment kuhusu ujumbe huo nilimpigia simu Wenje lakini hakupokea, baadae nikawapigia simu wabunge naofahamiana nao. Wakadhibitisha kuwa ule ujumbe ni wa Wenje alioutoa kwenye group lao la whatsapp liitwalo "CHADEMA MPs"

Baada ya kujiridhisha kuwa ujumbe ule ni wa Wenje nikawa kwenye position nzuri ya kuchangia, maana huwa najihadhari sana kuchangia taarifa ambayo siielewi vya kutosha (partial informed).

So kwa maoni yangu Wenje alikua sahihi kwa sababu alikotoa mawazo yake ni mahali sahihi. Group ya wabunge wa CHADEMA ni sawa na kikao cha wabunge wa chadema. So ni kikao kama vilivyo vikao vingine vya chama. Tofauti tu ni kuwa kikao hiki kinafanyika online.

So hiki ni kikao cha uongozi cha chama hata kama hakikua rasmi. Ndani ya vikao kama hivi ni kawaida kuwa na mawazo tofauti baina ya wajumbe. Yani kupingana kwa hoja lakini mwisho wa kikao wanatoka na msimamo mmoja na msimamo huo ndio unaoenda kwa wananchi.

Sasa Wenje ndani ya kikao kile alikua na mawazo tofauti na wenzie. Hii si dhambi, maana ni kawaida ya vikao. Na baada ya majadiliano makali Wenje na wengine waliokua na mtizamo tofauti wakakubaliana na maamuzi ya chama ya kumvua uanachama Zitto maana ni ya kikatiba.

So hadi hapo Wenje hana kosa. Kosa lipo kwa aliyevujisha taarifa hiyo ya kikao cha ndani na kuileta public. Huyu ndiye anayepaswa kuadhibiwa.

Kuvujusha taarifa ya vikao vya ndani ya mjumbe mwenzio kisa tu hujakubaliana nae mawazo, ni kosa kubwa katika maadili ya uongozi.

Mbona kuna mgogoro kwenye baraza la mawaziri na wapo ambao hawamtaki Pinda, lakini je ni waziri gani amewahi kumrekodi mwenzie asiyekubaliana nae mawazo na kurusha mtandaoni? Yani waziri anayemuunga mkono Pinda akamrekodi mwenzie anayemponda Pinda kisha akarusha mtandaoni.!

Kama hamna, sisi CHADEMA tunaojiona wakamilifu kuliko CCM hii tabia tumeipata wapi? Mbona hao CCM tunaowakosoa kila siku wanatushinda maadili?

Nashauri mbunge aliyehusika "kuscreen shot" ule ujumbe wa Wenje na kuusambaza achukuliwe hatua. Huyu hana sifa za kuwa kiongozi.

Kama ameweza kuvujisha taarifa ya kikao cha ndani kisa tu hakubaliani na aliyeitoa taarifa hiyo, huyu akipewa nafasi kubwa anaweza kuvujisha hata taarifa za kuitia nchi hatarini kisa hakubaliani nayo. Narudia, mbunge aliyehusika hafai kuwa kiongozi.!

JIPU LIMEPASUKA, SIWEZI KUWA ADUI KWA KUSEMA UKWELI.

Malisa GJ || Your Partner In Critical Thinking.!