Na Kijakazi Abdalla- Maelezo Zanzibar
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo amesema
hospitali za Zanzibar hazifanyi biashara ya vipimo vya aina yoyote katika
maabara zake bali huwataka wananchi kuchangia kwa baadhi ya vipimo hivyo na
kupewa risiti mara baada ya kuchangia huduma hiyo.
Hayo ameyaeleza wakati akijibu swali la mwakilishi wa Jimbo la Muyuni
Mhe. Jaku Hashim Ayoub katika ukumbi wa Baraza la Wawakilishi huko Chukwani
Wilaya ya Magharibi Unguja.
Amesema kuwa ipo haja kwa wananchi kudai risiti ya malipo wakati
wanapochangia huduma hiyo ili iwe ndio uthibitisho wa malipo hayo na endapo
ikitokea kwa mwananchi yoyote kutopewa risti hiyo kwa ajili ya huduma aliyochangia
anatakiwa kutoa taarifa kwa uongozi wa hospitali aliyolipia au kutoa taarifa
kwa watendaji wa wizara hiyo.
Aidha amesema kuwa uongozi wa Wizara hiyo hauna taarifa juu ya kuwepo kwa
wizi wa baadhi ya vifaa vya matibabu na kuuzwa kwa wananchi kutoka kwa
watendaji wa wizara hiyo hivyo amesema Wizara yake italifanyia kazi tatizo hilo
ipasavyo ili kulipatia ufumbuzi unaofaa na kuwataka wananchi kushirikiana na
Serikali kwa kutoa taarifa pindi wanapobaini kuwepo kwa tatizo hilo kwa maslahi
yao na Taifa kwa ujumla.
Wakati huohuo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwa kupitia
Wizara yake ya Biashara, Viwanda na Masoko inafanya juhudi za makusudi kwa
lengo la kuwasaidia Wajasiriamali kuweza kuuza bidhaaa zao katika masoko ya
ndani na nje Nchi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko Zanzibar
Mhe. Thuwaiba Edington Kisasi katika kikao cha Baraza la Wawakilishi huko
Chukwani Wilaya ya Magharibi Unguja, wakati akijibu swali la mwakilishi wa
nafasi za wanawake Mhe. Shadya Mohammed Suleiman.
Mhe. Kisasi amesema Wizara yake imekuwa ikichukuwa juhudi mbalimbali
katika kuzitafutia masoko ya nje bidhaa zinazozalishwa Zanzibar, juhudi hizo ni
pamoja na kutumia soko la Jumapili ambalo lilianzishwa rasmi huko Pemba kwa
Wajasiriamali wanaouza bidhaa zao ndani ya Kisiwa cha Pemba.
Aidha amesema kuwa Soko hilo lina jumla ya vikundi 28 hadi sasa ambavyo
vinashiriki kikamilifu katika maonyesho mbalimbali ya biashara pamoja na
kuandaa na kuratibu ushiriki Wajasiriamali wa Zanzibar katika maonesho hayo na
Matamasha ya Biashara ya ndani na nje ya Zanzibar.
Hata hivyo Naibu Waziri huyo amesema kuwa katika maonesho ya Sabasaba
yaliyofanyika Mwaka jana jumla ya wajasirmali 48 kutoka Zanzibar walishiriki
maonyesho hayo ambapo wajasiriamali 19 kutoka Pemba na 29 kutoka Unguja, pamoja
na hayo juhudi hizo zimeshaanza kuzaa matunda na wajasiriamali wameanza kupata
masoko zaidi kwa kwa ajili kuuza bidhaa zao.