Tuesday, 17 March 2015

Zitto: 'Kipengele kilichotumika kunifukuza Chadema kilitungwa kwa ajili yangu..'





MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amevunja ukimya baada ya kuzungumzia tuhuma mbalimbali ambazo zimekuwa zikielezwa juu yake, ikiwamo usaliti ndani ya chama chake na hatima yake ya siasa baada ya kutimuliwa.


Katika mahojiano haya, zitto anatoa maelezo yote juu ya tuhuma dhidi yake.
Swali: Mwaka 2009, ulitaka kugombea uenyekiti wa Chadema, uamuzi huo ulikuwa ni wako mwenyewe ama kuna watu nyuma yako walikushawishi kufanya hivyo?
Jibu: Chadema nilivyoingia kwenye uongozi Makao Makuu, kulikuwa na wabunge watano, wanne wa kuchaguliwa na mmoja wa viti maalumu.

Nilivyoingia pale nilipewa nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi na wa Mambo ya Nje kwa ajili ya kujenga mahusiano ya chama chetu na vyama vingine vya kimataifa, hiyo kazi niliifanya kwa ubora na mpaka sasa uhusiano wote ya Chadema na vyama vya nje, niliyajenga mimi.

Mwaka 2005 niliandika mkakati wa uchaguzi tukapata majimbo mengi zaidi, tulipata asilimia nane ya kura hivyo tukapata wabunge sita wa viti maalumu.
Kabla ya hapo Chadema ilikuwa ikizidiwa hata ya UDP, pamoja na kwamba kilikuwa na wabunge tangu 1995.

Wabunge wake hawakujitanabaisha kama wapambanaji wa misingi ya kitaifa, tulivyoingia (Bungeni) sisi na kina Ndesamburo (Mbunge wa Moshi mjini, Philemon Ndesamburo), DK Slaa (Katibu Mkuu wa Chadema Dk. Willibrod Slaa), tukaanza kubadilisha hali hiyo.
Tukaanza kupambana na ufisadi, kabla ya hapo Dk. Slaa alikuwa bungeni kwa miaka 10 lakini hakuwa machachari kama ilivyokuwa kuanzia 2005.

Alivyoingia mwaka 2005 ndipo tukaanza na hoja kama zile za EPA na Buzwagi.
Baada ya hapo mimi na kina Profesa Kitila Mkumbo tukaona kuna haja ya kubadilisha chama, mwaka 2009 nilivyotaka kugombea uenyekiti nilikuwa na nia ya dhati kabisa.

Ndani ya Chadema kuna watu wanaamini katika uliberari, kama biashara na mtaji, hawa ni watu kama kina Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe), sisi tunaamini katika demokrasia ya jamii. Hapa kwenye kundi hili unatukuta mimi kina Profesa Mkumbo, Profesa Mwesiga Baregu, na wenginr, tulitaka kukitoa chama kwenyel mrego wa kihafidhina kwenda kwenye ujamaa.
 
Hata hivyo wazee walinitaka niache kugombea nikaacha, ni kweli ukiangalia chanzo cha ugonzi ni mwaka 2009, ila mimi sikudahani kama kitu kile kingeleta chuki, nilidhani mambo yangeishia pale.

Swali: Nini kilifanya iwe vigumu kumaliza tofauti zako na Chadema?
Jibu: Mara zote nimekuwa nikiwaambia Chadema kwanza waniambie kosa langu ni nini, Ndesamburo aliwahi kunifuata ili tuyamalize, Wenje naye alinifuata na siku kutaka tuyamalize, lakini upande mwingine viongozi nao wanasema yao kwa hiyo ni undumilakuwili tu kila mahali.

Swali: Kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa wewe na Mbowe mna ugomvi binafsi, tofauti na vile ambavyo watu wanadhani kuwa mnagombea uongozi. Wengine wanasema uliwahi kutoa siri zake, juu ya kuwa na nyumba Dubai, madai haya yana ukweli?
 
Jibu: Kama Mbowe ana mali nje mimi kwa kweli sijui, mimi nilitoa hoja ikaundwa kamati ya uchunguzi, kama ilimkuta ana mali nje sijui.
 
Hata hivyo kama ana nyumba, ama mali nyingine ni kwa nini auogope? Kama una nyumba Marekani, Afrika Kusini, Dubai ama wapi hiyo siyo tabu, ilimradi kwenye tamko la maadili (Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma) uwe umesema kuwa unazo na TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wajue umepata wapi hizo fedha.

Swali: Lakini inadaiwa kuwa ulikaa na Mbowe wewe akakueleza kama mtu wake wa karibu kuwa ana nyumba Dubai na wewe ukatoa hizo habari kwa umma na ndicho kilichomuudhi.
 
Jibu: Mimi sijawahi kukaa na Mbowe kuzungumza hayo mambo. Sina ugomvi binafsi Mwenyekiti wa Chadema, siku zote nimekuwa nikimchukulia kama kaka, ndiyo maana hata akinishambulia nimekuwa nikijitahidi kukaa kimya.
 
Mwanzoni kabisa yeye alikuja chuo kikuu kunifuata, mwanzoni mwa mwaka 2001, nikiwa mwanachama wa Chadema lakini siyo kiongozi, yeye akiwa Mbunge wa Hai, alikuja akaniambia naomba tuzungumze utusaidie kwenye chama.

Alikuwa anataka kufanya mabadiliko ya katiba ya chama, nikatumia nafasi yangu ya uanaharakati wa wanafunzi na uwezo wangu wa uchambuzi tukafanya hivyo tulivyofanya.
Tukabadilisha chama mimi na yeye, mabadiliko makubwa ambayo yanaonekana hivi sasa Chadema ni kazi ambayo tulifanya mimi na yeye, hata gumboe mwaka 2009 niliona ni jambo la kawaida. Kilichopo ni mitizamo tofauti ya namna ya kuendesha siasa, na tofauti hizo zimesababisha yatokee yaliyotokea.
 
Wakati mwingine nikikaa peke yangu huwa yangu na kujiuliza, huwa sioni msingi wa ugomvi wangu na chadeama, naona ni ugomvi tu wa madaraka na juhudi za watu kutaka kuondoa wengine katika ulingo.
Katika mazingira kama hayo ni rahisi kutoa tafsiri kwamba kuna ugomvi binafsi.

Yeye (Mbowe) alikuja hapa Kigoma akafanya mkutano wa hadhara akanitukana, akasema alinisaidia sijui gari, sijui nini, yaani alikuja nyumbani kwetu kunisimanga.
Nikasema huyu mtu ananisimanga, kwanza ni mambo ya kishamba, kwamba unamsaidia mtu halafu unakuja kumsema, kwanza kuna vitu ambavyo mimi mwenyewe nimemsaidia labda kifedha ama siyo fedha, na tunajua kati ya mimi na yeye.

Siyo vitu naweza kuibuka nikasema nilimdharau sana kwa kweli, na juzi nimemsikia huko Shinyanga akisema kuwa hawezi kukaa na kuongea na mimi kwamba ni msaliti na mambo kama hayo. Huu ni undumilakuwili kwa kweli kwa sababu huku anatuma watu kwamba kina Ndesamburo (Philemon Ndesamburo), kwamba tuongee tuone namna ya kuyamaliza haya mambo alafu yeye huku nyuma akikaa anaongea yake.
Kwa hiyo binafsi naamini sina ugomvi naye sanasana ni tofauti za kiitikadi. Mimi na yeye tumekaa Bungeni miaka 10, naomba tu watu watupime.

Katika miaka yangu 10 ni hoja gani nimezisimamia na yeye ni zipi amezisimamia.
Mimi siku zote siasa zangu ni hoja na issue za kusaidia wananchi na nafurahi ninavyosimamia vitu na kuona vikienda.

Swali: Mara kadhaa viongozi wa chama chako wamekuwa wakikutuhumu kwa kusaliti chama, na kwamba kwa upande mmoja unatumiwa na CCM na upande mwingime usalama wa taifa, ni kwa nini ushutumiwe kwa tuhuma kama hizo?
 
Jibu: Kwenye siasa ukitaka mwanasiasa amalizike ni kumpa hizo tuhuma. Lakini waulize (Chadema), ni taarifa zipi zinapelekwa kwenye usalama wa taifa, watu haohao walisema siendi kwenye vikao vya chama, wala ofisini, sasa hizo taarifa ninazozipeleka ni zipi wakati kwenye vikao wala ofisini siendi? Mtu anayepeleka taarifa ni yule asiyekosa kwenye vikao. Anahudhuria kila kikao ili apate taarifa za kupeleka.

Lakini pia angalia, mwaka 2010 nilitoa taarifa ya kumuomboa Waziri Mkuu, hoja ile ikaungwa mkono kwa kusainiwa na wabunge wa pande zote, hivyo ikasaidia kuondoa baadhi ya mawaziri waliokuwa na shutuma.
Mwaka 2013 kulikuwa na Operesheni Tokomeza. Ripoti ya Kamati ya Bunge iliyokuwa imewasilishwa ilikuwa inamtaja waziri mmoja tu, lakini nilisimama na kujenga hoja mawaziri wengi tu wakaondolewa.

Mwaka 2014 nimepeleka hoja ya Escrow na nikaisimamia, mawaziri wameondoka, serikali imetikisika, sasa mtu anayetumika na Chama Cha Mapinduzi kwa nini aiangushe serikali ya chama hicho mara tatu ndani miaka mitano? Mtu ambaye anatumika inawezekanaje alete mjadala utakaoingusha serikali?
Ndiyo maana sipotezi muda kujibizana na propaganda za aina hiyo, watuambie ni taarifa gani zilipelekwa huko zikawaathiri?

Swali: Baada ya Mahakama kutoa uamuzi wake na Mwansheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lisu kutangaza kuwa umefukuzwa uanachama kwa kuwa kukishitaki chama ni kujifukuza katika chama moja kwa moja, tangu ukiwa kiongozi wa chama uliwahi kukitilia shaka kifungu hicho kwa kuwa hivi sasa umeonekana kukilalamikia.

Jibu: Hiki kifungu kipo kwenye kanuni na wala siyo Katiba, kilitungwa mwaka 2013. Mwaka huo kuna mabadiliko fulani fulani yalifanywa. Mabadiliko yale yalikuwa na malengo fulanifulani ikiwamo kulenga watu fulanifulani.
 
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri, mamlaka ya kutoa haki iko kwenye chombo kimoja tu nacho ni Mahakama, kila raia ana haki ya kwenda mahakamani kudai haki, unaposema mwananchama wa Chadema akienda mahakamni amejivua uanachama ina maana wewe huitambui Katiba ya Jamuhuri.
 
Hii ina maana kama mwanachama amekipangisha chama, na chama kikashindwa kulipa kodi, yule mwanachama akienda mahakamani amejivua mwenyewe uanachama kwa kuwa haruhusiwi kwenda mahakamani.

Hicho ni kipengele ambacho hakikupaswa kuwap, Wanachama wa Chadema waende mahakamani kushtaki kipengele hicho ili kitangazwe kuwa siyo halali.
Chama kinachopambana kushika dola hakipaswi kuwa na vipengele kama hivi. Ila yote kwa yote hiki kipengele kimewekwa mwaka 2013 na mwaka 2015 kikatumika kwangu, ni wazi kilitungwa kwa ajili yangu.

Swali: Baada ya kufukuzwa Chadema, ni nini hatma yako kisiasa?
Jibu: Nina ziara ya kuzunguka na wananchi wa jimbo langu kuangalia jinsi ya kuwatumikia, leo (jana) nawaaga rasmi kwamba sintakuwa nao baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, lakini ni nini kinachokuja baadaye ya hapo tutakijua vizuri wiki ijayo (wiki hii).
 
Hatujajua kama Chadema wameandika barua kwa Spika ili kunitangaza kuwa jimbo liko wazi, kama ndivyo tutakaa kujua ni nini cha kufanya.
Ilipaswa baada ya kesi kwisha taratibu zifuatwe, mpaka sasa sijapata taarifa zozote za kufukuzwa ndiyo maana nasema mpaka wiki kesho iishe tutajua, nitakuwa na nia ya kuendelea kutumikia kwenye jimbo lolote Oktoba.

Swali: Una mpango wa kujiunga na ACT?
Jibu: Tusijaribu kuvuka mto kabla hatujafika pa kuvukia.
 
Swali: Vipi hukumu ya Mahakama Kuu juu ya kesi yako na Chadema?
Jibu: Kwenye kazi yangu kuna miguu ya watu wengi naikanyaga, taarifa yangu ya 

Escrow nimewakanyaga mpaka mahakama. Kwa hiyo yawezekana kabisa mahakama iliona hapa ndipo kwa kunikanyaga, ama yawezekana kabisa ni taratibu.

Inaonekana kuna uhusiano wa karibu wa mahakama na wanasheria wa Chadema, sisi tulisikia kwenye vyombo vya habari kwamba hukumu ya kesi yetu imetolewa.
Hata baada ya hukumu hiyo, tulijaribu kufuatilia ili kupata hukumu, kwa siku mbili tulizungushwa, siku ya tatu tukaambiwa kuwa jalada lipo kwa jaji kiongozi.
Lakini mimi bado nina imani kwamba wakuu wa mahakama watachunguza jambo hili na kuona kama kuna cha kufanya.

Sisi tulipaswa kuitwa mahakamani, lakini hatukuitwa, kuna taratibu za mahakama hazikufuatwa, tuna imani kuwa viongozi wa mahakama watachunguza kama kuna suala la rushwa katikati hapa ama kuna nini.

Lakini pia hali hii imenifanya niwe na kiu zaidi ya kuhakikisha nikipata tena nafasi nitafanya operesheni kwenye mfumo wa mahakama kwa kuwa umekuwa na malalamiko sana ya kuwaumiza wananchi.