Sunday, 21 June 2015

Mji Mkongwe wa Zanzibar wawekewa mtandao wa CCTV kamera




Zanzibar inatarajia kuimarika zaidi kiulinzi na kiusalama sambamba na kuongeza mapato yake kupitia sekta ya utalii baada ya kukamilika kwa mradi muhimu wa kamera za kurikodi matukio ya kila siku (CCTV CAMERA) zinazofungwa katika eneo la Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Mradi huo muhimu wa mfumo wa ‘CCTV Camera’ uliofadhiliwa na Kampuni ya Mawasiliano ya Kisasa ya ZTE kutoka nchini China ni utekelezaji kufuatia ziara ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi aliyoifanya nchini China mwishoni mwa mwaka jana.


Balozi Seif, alipata fursa ya kukagua kituo cha mradi huo (Comanding Post) kwenye ofisi zake za Malindi, mjini Zanzibar na kujionea teknolojia mpya itakayotumika katika kuziongoza kamera hizo.

Katibu wa Kamati ya Wataalamu ya Usimamizi wa Mradi wa CCTV Camera, Jabir Haji Abdulla alimueleza Balozi Seif kwamba mradi huo unatarajiwa kuwa na kamera 300 lakini zitakazofungwa kwa sasa ni kamera 150 ambapo hadi sasa kamera kumi tayari zimeshafungwa.

Jabir alisema kituo hicho kitakachokuwa chini ya uangalizi wa Idara zote za vikosi vya ulinzi vya Zanzibar, likiwemo Jeshi la Polisi, Usalama wa Taifa na KMKM hivi sasa tayari kina uwezo kamili wa kurikodi matukio mbalimbali yanayotokea katika eneo la Mji Mkongwe.

Katibu huyo alisema kwamba, kamera za mradi huo zina uwezo wa kuvuta tukio kwa zaidi ya mita 150 zitasaidia kurikodi matukio ya uhalifu kama ujambazi na makosa ya barabarani yanayofanywa na madereva wazembe pamoja na kuongoza misafara ya Viongozi Wakuu.

Alifahamisha kwamba katika kuimarisha hali ya usalama ndani ya Mji wa Zanzibar, upo mradi mwengine unaotarajiwa kusimamiwa na Kampuni ya ZEST utakaohusisha maeneo ya kwa Bakhresa, Mlandege pamoja na Nyumba za Maendeleo za Michenzani.

“Kamera hizi zina uwezo wa kuzunguuka pembe zote (360%) zina uwezo wa kuvuta tukio lolote kwa zaidi ya mita 150 na kuufanya mji kuwa salama,” alisema Jabiri.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, aliipongeza Kampuni ya ZTE kwa jitihada ilizochukuwa za kutekeleza kwa vitendo ahadi waliyompa kuanzisha mradi huo wakati wa ziara yake nchini China.

Balozi Seif alisema serikali ilipaswa kuwa na mradi huu muhimu kwa muda mrefu uliopita hasa ikilinganishwa na matukio mbali mbali yaliyowahi kutokea hapa nchini likiwemo la hujuma dhidi ya wageni wanaotembelea maeneo ya utalii.

Alisema matumaini yake ni kwamba mradi huo kwa kiasi kikubwa utakapokamilika utasaidia kupunguza matukio tofauti ya uhalifu, ujambazi pamoja na ajali za kizembe zinazotokea barabarani.

Mradi huo wa kamera za kurikodi matukio mbali mbali ya kila siku (CCTV CAMERA) ndani ya mji wa Zanzibar, umeelezwa kuwa wa mwanzo kuwekwa ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki.