WAJUMBE WA Baraza la
Wawakilishi wameitaka Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kusimamia Uchaguzi
Mkuu kwa kufuata misingi ya sheria na katiba ili kuepuka vurugu.
Wakichangia makadirio
mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa
Rais, Mwakilishi wa Jimbo la Wete, Asaa Othman alisema vurugu za kisiasa
Zanzibar hujitokeza kipindi cha Uchaguzi Mkuu na mara Tume inapotangaza matokeo
ya urais.
Alisema matarajio ya
wananchi wengi, kuona ZEC iliyopewa jukumu la kusimamia uchaguzi inatekeleza
majukumu yake kwa kufuata matakwa ya kikatiba na sheria na sio kuhubiri ushabiki
wa kisiasa.
“Mwaka huu tunakabiliwa na
matukio mawili makubwa Kura ya Maoni ya Katiba Inayopendekezwa pamoja na
Uchaguzi Mkuu ambapo matarajio yetu makubwa kuona utulivu wa kisiasa
unadumishwa katika kipindi chote hicho na kuepuka
matukio ya fujo,” alisema Mhe
Asaa.
Mwakilishi wa Jimbo la
Micheweni, Subeit Khamis Faki (CUF) aliitaka ZEC kusimamia uchaguzi kama
ilivyofanya katika mwaka 2010, ambapo matukio ya fujo na vurugu za kisiasa
zilidhibitiwa.
Aidha aliitaka Tume ya
Uchaguzi kusimamia vizuri kazi za uandikishaji na uboreshaji wa daftari la
kudumu la wapiga kura ambalo litawawezesha wananchi kutumia haki ya
kidemokrasia kupiga kura.
Aliitaka tume kufanya kazi
ya kuwaandikisha wapiga kura wenye sifa ya kushiriki katika uchaguzi mkuu, na
wale ambao hawastahiki wasiorodheshwe.
“Kazi ya uboreshaji wa
daftari la kudumu la wapiga kura imeanza katika kisiwa cha Pemba, lakini
tunaiomba ZEC kuhakikisha kwamba watu wenye sifa tu ndiyo wanaoandikishwa
katika daftari hilo,” alisema Mhe Subeit.
Mwakilishi wa Viti
Maalumu, Mwanaidi Kassim Mussa (CCM) aliipongeza Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar
kwa kufanya kazi za kusimamia daftari la kudumu la wapiga kura vizuri.
Alizitaja miongoni mwa
kazi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ni kuboresha daftari la kudumu la
wapigakura ambalo litatoa nafasi kwa wananchi kushiriki katika uchaguzi mkuu wa
mwaka huu.
“Tunaipongeza Tume ya
Uchaguzi ya Zanzibar kwa kufanya kazi zake vizuri ambazo zimeiwezesha kusimamia
uchaguzi mkuu vizuri kwa mafanikio mwaka 2010,” alisema Mhe Mwanaidi.
Mwakilishi wa Jimbo la
Amani, Fatma Mbarouk Said (CCM) aliitaka Serikali kudhibiti amani na utulivu
kuelekea katika uchaguzi mkuu kwa ajili ya kuhakikisha makundi ya wanawake na
watoto yanakuwa salama.
Alisema uzoefu unaonesha
kwamba katika fujo za uchaguzi mkuu waathirika wakubwa ni wanawake na watoto
kutokana na mazingira yao kwa ujumla:
“Tunaiomba Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kudhibiti amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu kwa
ajili ya kuhakikisha kwamba jamii yetu inakuwa salama ikiwemo wanawake na
watoto,’’ alisema Mhe Fatma.
Mwakilishi wa Viti
Maalumu, Panya Ali Abdallah (CCM) amewataka baadhi ya wanasiasa kuacha
kuingilia majukumu ya Tume ya Uchaguzi.
Alisema katika siku za
hivi karibuni wapo viongozi wa kisiasa ambao wamekuwa wakitoa kauli za
kushutumu majukumu ya tume iliyopewa kwa mujibu wa katiba na sharia:
“Mheshimiwa Spika nawaomba
viongozi wa vyama vya siasa kuacha kutoa kauli za shutuma kwa taasisi iliyopewa
majukumu ya kusimamia uchaguzi mkuu (ZEC) kwani kufanya hivyo ni sawa kuinyima
uhuru wa majukumu yake,’’ alisema Mhe Panya.