Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon
WANAJESHI wawili wa
Tanzania ambao wako kwenye jeshi la kulinda amani la Umoja wa Mataifa Mashariki
mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wameuawa katika vita na waasi wa
eneo hilo.
Taarifa iliyotolewa na
Ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN) nchini, ilifafanua kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa
Mataifa, Ban Ki-moon, amelaani mauaji ya wanajeshi hao na tayari ametuma salamu
za rambirambi kwa Serikali pamoja na familia za wapiganaji hao mashujaa wa
Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Katika tukio hilo,
wanajeshi wengine 13 wa DRC walijeruhiwa vibaya huku wanajeshi wengine wanne
hawajulikani waliko.
Tukio hilo lilitokea jana
Mashariki mwa DRC, ambako majeshi ya Tanzania yako kwenye vikosi vya Umoja wa
Mataifa vya kulinda amani katika eneo hilo, ambalo limekuwa linashambuliwa mara
kwa mara na waasi wa DRC.
Taarifa iliyotolewa jana
na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ilieleza kuwa askari hao ambao ni sehemu ya
Wanajeshi ya Kikosi Maalumu cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa (MONUSCO),
walifikwa na mauti wakati wakiwa katika shughuli zao za kila siku na mara
msafara wao ulishambuliwa na wapiganaji wa kikundi cha waasi cha ADF.
UN kwenye taarifa yake
wameutaja mji ambako wanajeshi hao walikuwa kuwa ni Beni, uliopo Kaskazini mwa
Jimbo la Kivu. Taarifa hiyo ilisema wanajeshi hao, walishambuliwa wakati wakiwa
kwenye shughuli za kuwalinda raia.
Shambulio hilo limekuja
zikiwa ni siku chache baada ya helikopita iliyokuwa na wanajeshi ya Monusco,
kushambuliwa kwa risasi na wapiganaji wa waasi kutoka eneo hilo.
Ki-moon pia amelaani
kitendo cha waasi wa ADF kuendelea kuwashambulia raia katika eneo hilo la Beni.
Umoja wa Mataifa umekuwa unatoa
ulinzi katika maeneo ya Mashariki mwa DRC kwa lengo la kuwalinda raia na kuuzia
mashambulizi dhidi ya waasi. Ki moon pia ametoa salamu za pole kwa familia za
wanajeshi hao pamoja na Serikali ya Tanzania