JUMUIYA ya Kimataifa
katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) jijini hapa, imeelezea msimamo wake
thabiti wa kuunga mkono kwa dhati na kwa kila hali kazi na jukumu ya Jopo la
Watu Mashuhuri Duniani la Kukabiliana na Majanga Duniani linaloongozwa na Rais
Jakaya Kikwete.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh.Jakaya Kikwete
Jumuiya hiyo imeeleza
msimamo wake wa kuunga mkono Jopo hilo wakati Rais Kikwete na wana-Jopo wenzake
walipopata nafasi ya kuwaelezea Wawakilishi wa Kudumu wa nchi mbali mbali
duniani katika Umoja wa Mataifa kuhusu kazi iliyofanywa na Jopo hilo katika siku
za mwanzo kabisa.
Jopo hilo lililotangazwa
na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon Aprili 2, mwaka huu,
limepewa jukumu ya kupendekeza jinsi gani dunia inavyoweza kukabiliana na
majanga ya kiafya duniani, na hasa magonjwa ya milipuko, kama ilivyokuwa ebola
katika nchi za Afrika Magharibi za Guinea, Liberia bna Sierra Leone.
Baada ya wiki moja ya kazi
kubwa mjini New York, Rais Kikwete na wajumbe wa Jopo hilo kutoka Brazil,
Botswana, Indonesia, Uswisi na Marekani, walikutana na Wawakilishi wa Kudumu wa
mataifa mbali mbali katika UN kuwaelezea nini kimefanyika na nini kinatarajia
kufanyika.
Baada ya maelezo ya
wajumbe wa Jopo, mwakilishi wa Ubalozi wa Ujerumani katika UN alisema kuwa
Ujerumani inaunga mkono moja kwa moja kazi ya Jopo hilo akisisitiza kuwa
Kiongozi wa Ujerumani, Kansela Merkel amekubali kutoa kiasi cha dola za
Marekani milioni moja (sh bilioni 1.9) kuunga mkono shughuli za Jopo hilo.
Mwakilishi wa Senegal
alisema kuwa nchi yake inaunga mkono moja kwa moja kazi ya Jopo hilo lililoteuliwa
na Katibu Mkuu wa UN, akisisitiza kuwa Senegal, kama Mwenyekiti wa Kamati ya
Oslo ya Afya katika Umoja wa Mataifa itashirikiana na Jopo hilo moja kwa moja.
Mwakilishi wa Ufaransa
alisema kuwa nchi yake inaunga mkono kazi ya Jopo moja kwa moja na kuwa ni
uamuzi wa busara wa Katibu Mkuu wa UN kuunda Jopo hilo.
Mwakilishi wa Uingereza
alipokea kwa mikono miwili uundwaji wa Jopo hilo, akisisitiza kuwa nchi hiyo
itaendelea kuunga mkono jitihada za Jopo hilo kama ilivyoiunga mkono Sierra
Leone wakati wa kukabiliana na ebola.
Mwakilishi wa Luxembourg
alisema kuwa dunia inalitarajia Jopo hilo kuelekeza nguvu yake katika
mapendekezo ya uongozi kuliko changamoto za kiufundi.
Aidha, ameongeza kuwa nchi
hiyo baada ya kushika Uenyekiti wa Umoja wa Ulaya (EU) itaongeza kazi yake
katika kuchunguza athari za ebola na kiini chake.