MAMIA ya wakazi wa Dar es
Salaam leo wanatarajia kutoa heshima za mwisho kwa John Nyerere (58), ambaye ni
mmoja wa watoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
John alifariki dunia juzi
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alikokuwa amelazwa.
Makongoro Nyerere ambaye
ni mtoto mwingine wa Mwalimu Nyerere, alisema Dar es Salaam jana kuwa mwili wa
John utasafirishwa kesho kwenda Mwanza na kisha kupelekwa kijijini kwao Butiama
Mkoa wa Mara kwa maziko.
“Misa ya kumuombea John
itafanyika hapa Msasani nyumbani kwa Mwalimu na kufuatiwa na utoaji wa heshima
za mwisho,” alisema Makongoro, ambaye ni Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki.
John alitumikia Jeshi la
Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na alishiriki Vita vya Kagera vya 1978 na
1979, vilivyolenga kumng’oa nduli Iddi Amin wa Uganda.
Watoto wengine wa Mwalimu
ni Andrew, Magige, Madaraka, Anna na Rose.