RAIS Jakaya Kikwete
ameitisha mkutano wa wakuu wenzake wa nchi tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC) ili kujadili hali ya Burundi.
Ameitisha mkutano huo
wakati Burundi ikiripotiwa kuwa katika vurugu zinazotishia hali ya usalama,
hasa kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi ujao.
Rais Kikwete amechukua
uamuzi huo kwa wadhifa alionao wa Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi
Wanachama wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Alitangaza kuitisha
mkutano huo wakati alipozungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya
Umoja wa Mataifa (UN), kuwaelezea matokeo ya mkutano wa wiki moja wa Jopo la
Watu Mashuhuri Duniani, linaloangalia jinsi dunia inavyoweza kukabiliana na
majanga ya kiafya katika siku zijazo kufuatia balaa la ugonjwa wa ebola katika
Afrika Magharibi.
Rais Kikwete na wana-Jopo
wenzake walizungumza na wanahabari juzi jijini New York, baada ya kuwa
wamemaliza kikao cha kwanza cha Jopo lao lililoteuliwa na Katibu Mkuu wa UN,
Ban Kimoon, Aprili 2, mwaka huu, 2015, kupendekeza jinsi dunia inavyoweza
kukabiliana na majanga ya kiafya, na hasa ya magonjwa ya mlipuko, katika siku
zijazo kufuatia balaa na athari za ugonjwa wa ebola katika Afrika Magharibi.
Ugonjwa wa ebola umeua
watu karibu 10,000 katika kipindi kifupi katika nchi za Guinea, Liberia na
Sierra Leone. Ugonjwa huo ulijitokeza kwa mara ya kwanza mwaka 1976, karibu miaka
40 iliyopita katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mpaka sasa ugonjwa huo
hauna dawa inayojulikana dhahiri wala chanjo. Katika maswali yaliyofuatia
maelezo yake na ya wanajopo wenzake kuhusu kazi yao ya wiki moja, Rais Kikwete
aliulizwa kuhusu hali ilivyo katika Burundi na Tanzania, kama jirani inachukua
hatua gani kukabiliana na hali hiyo katika nchi jirani.
Rais Kikwete alisema baada
ya mawaziri wa nchi za nje wa Tanzania, Kenya,
Uganda na Rwanda kuwa
wametembelea Burundi majuzi, kwa maelekezo yake, na kumaliza ziara yao kwa
kujionea hali ilivyo katika nchi hiyo, ameamua kuitisha Mkutano wa Wakuu wa
Nchi za EAC jijini Dar es Salaam, ambako mawaziri hao watatoa ripoti yao ili
ijadiliwe.
“Tumekubaliana kuwa sisi
ndani ya EAC – Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi yenyewe tukutane Dar
es Salaam, Jumatano ijayo, Mei 13 (keshokutwa), ili tujadiliane jinsi gani ya
kuwasaidia ndugu zetu wa Burundi kuandaa uchaguzi wao kwa mafanikio,
wakihakikisha kuwa nchi yao inabakia na umoja, utulivu, usalama na amani bila
misukosuko isiyokuwa na sababu,” Rais Kikwete aliwaambia waandishi hao wa
habari.
Rais Kikwete aliongeza:
“Baada ya hapo, tutaweza sasa kuwaelezea nyie waandishi wa habari kuhusu
msimamo wa EAC na hata msimamo wa Tanzania kuhusu Burundi – tuwe na subira na
tunaamini kuwa Burundi itaendelea kuwa ya utulivu na amani.”
Katika siku za karibuni,
kumekuwepo na hali ya mjadala mkali kuhusu maana halisi hasa ya Katiba ya
Burundi, hususani katika kipengele kinachohusu vipindi vya kutumikia Urais.
Baadhi wamekuwa wanadai
kuwa kwa kutumikia miaka 10, Rais wa sasa, Pierre Nkurunziza amekamilisha
mahitaji ya kikatiba. Wengine wanasema kuwa bado anayo haki ya kugombea kwa
kipindi kimoja zaidi, kwa sababu Rais amechaguliwa mara moja tu na wananchi.
Chama chake cha CNDDFDD
kimempitisha tena kuwa mgombea urais na wiki iliyopita Mahakama ya Katiba,
ilisema Rais Nkurunziza anayo haki ya Kikatiba kuwania nafasi hiyo kwa mara
nyingine.
Hali ilivyo Burundi Kwa
ujumla, wapinzani wa Rais Nkurunziza wameendelea kufanya maandamano bila kikomo
ya kumpinga kuwania urais kwa awamu ya tatu katika uchaguzi mkuu wa Juni.
Kutokana na maandamano
hayo yaliyodumu kwa wiki mbili, hadi sasa watu 18 wameuawa tangu Rais
Nkurunziza atangaze nia yake hiyo, huku maelfu wakiimbia nchi yao kwenda
kujisalimisha katika nchi jirani.
Kwa upande wa Tanzania,
zaidi ya Warundi 15,000 wameripotiwa kuingia wakipitia mpaka wa kijiji cha
Kagunga Kigoma Vijijini, ambako baada ya kupokewa wanapelekwa moja kwa moja
katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wilayani Kasulu.
Wakimbizi wengine
wanaingia nchini kupitia mpaka wa Ngara na Misenyi, ambako hata hivyo
wametakiwa kurejea makwao baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, John Mongela kusema
kwa sasa hakuna maandalizi yaliyofanywa kuwapokea wageni hao