Timu ya taifa ya soka ya Tanzania, Taifa Stars
imebanduliwa nje ya michuano ya COSAFA kuwania taji la kusini mwa nchi za
Afrika baada ya kufungwa na Madagascar mabao
2 kwa 0 Jumatano usiku wiki hii.
Tanzania imepoteza mchuano wake wa pili katika michuano
hiyo baada ya kufungwa na Swaziland katika mchuano wa ufunguzi kwa bao 1 kwa 0.
Madagascar ilipata mabao yake katika dakika ya 14
kupitia mchezaji Rakotoharimalala huku Randrianmanjaka akifunga la pili katika
dakika 44 ya kipindi hicho dakika moja kabla ya mapumziko.
Mashabiki wa soka nchini Tanzania wamesikitishwa na
matokeo hayo hasa kwa kufungwa na Madagascar na Swaziland ambazo zipo chini
yake katika orodha ya Shirikisho la soka duniani FIFA.
Mwenyekiti wa Shirikisho la soka nchini Tanzania TFF
Jamal Malinzi amesema licha ya kusikitishwa na matokeo hayo, sio mwisho wa soka
nchini humo.
“
Kuvunjika koleo sio mwisho wa uhunzi ”, Jamal Malinzi
amenukuliwa katika ukurasa wake wa Twitter.
Vijana wa Stars chini ya kocha Mholanzi Mart Nooij
wanasubiri sasa mchuano wake wa mwisho dhidi ya Lesotho kesho Ijumaa kabla ya
kurudi jijini Dar es salaam.
Wachambuzi wa soka wanasema huenda TFF ikamchukulia
hatua kocha Nooij kwa kushindwa kufanya vizuri katika michuano hiyo.
Katika matokeo mengine, Swaziland waliwashinda Lesotho
mabao 2 kwa 0 na kundi hilo linaoongozwa na Madagascar kwa alama 6 sawa na
Swaziland lakini Lesotho na Tanzania hazina alama yoyote.
Michuano ya mwisho ya kundi la A inachezwa leo Alhamisi
na mshindi kati ya Zimbabwe na Namibia atafuzu katika hatua ya robo fainali
lakini Ushelisheli inaweza kufuzu ikiwa itapata ushindi wa mabao mengi dhidi ya
Mauritius ikiwa Zimbabwe itawashinda Namibia.