Monday, 25 May 2015

RAIS ZUMA ATAKA UMOJA NA MSHIKAMANO BARANI AFRIKA

Rais JACOB ZUMA wa AFRIKA KUSINI ametoa wito wa kuwepo kwa umoja na mshikamano zaidi Barani Afrika ili kulifanya bara hilo liwe na matumaini kwa vijana na vizazi vijavyo. 

Katika hotuba ya kuadhimisha Siku ya Afrika Mjini PRETORIA Rais ZUMA amesema siku hii ni ya kutazama mambo ya mbele na kutathmini changamoto zilizopo barani humo. 

Akiwahakikishia wageni kutoka nchi mbalimbali za Afrika usalama wa kuishi na kufanya kazi nchini AFRIKA KUSINI Rais ZUMA amesema wananchi wa AFRIKA KUSINI na raia wa kigeni waliotoka nchi zingine za Afrika kutafuta fursa nchini humo wamekuwa na mshikamano na wanapaswa kuendelea na umoja huo kwa amani. 

Rais ZUMA amesema Siku ya Afrika pia ni kumbukumbu ya namna AFRIKA KUSINI ilivyopokea msaada na mshikamano kutoka nchi zingine za Afrika wakati wa mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi.

Maadhimisho haya ni ya 52 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika -OAU mwaka wa 1963.