Watu 18 wamekufa papo hapo kwa kuteketea kwa moto na wengine 11
wamejeruhiwa vibaya kutokana na basi walilokuwa wakisafiria kugongana na lori
aina ya Mitsubishi Fuso, katika kijiji cha Msimba tarafa ya Mikumi, barabara
kuu ya Morogoro – Mbeya.
Ajali hiyo imehusisha basi la Kampuni ya Nganga linalofanya safari
zake kutoka Wilaya ya Kilombero kuelekea mkoani Mbeya na kugongana na lori
hilo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonald Paulo alisema ajali
hiyo ilitokea jana saa mbili asubuhi katika eneo hilo huku likihusisha basi aina
ya Scania lenye namba za usajili T373 DAH na Fuso lenye namba za usajili T164
BKG.
Alisema chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi la Nganga ambaye
alikuwa katika mwendo kasi na kulipita gari lililokuwa mbele yake bila ya
tahadhari na kukutana na lori hilo na kisha kugongana nalo katika eneo hilo.
Alisema baada ya magari hayo kugongana, ndani ya buti ya basi
kulikuwa kumepakiwa pikipiki ambayo ilikuwa na mafuta na baada ya kutokea ajali
hiyo kulitokea mlipuko wa moto na kusababisha basi hilo pamoja na lori kuwaka
moto.
Kamanda huyo alisema kuwa kutokana na moto huo, baadhi ya abiria waliokuwepo
katika basi hilo walishindwa kujiokoa na hivyo miili yao kuteketea kabisa na
moto huo, wakiwemo madereva wote wa magari hayo.
Alisema majeruhi 11 wa ajali hiyo wamekimbizwa katika Hospitali ya
Mtakatifu Kizito iliyopo tarafa ya hiyo Mikumi kupatiwa matibabu huku hali zao
akieleza kuwa baadhi yao ni mbaya kutokana na kuungua vibaya kwa moto.
Kamanda huyo alisema miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika
hospitali hiyo ambapo mpaka sasa haijatambulika majina yake, licha ya madereva
wa magari yote kufa.
Hata hivyo, Kamanda huyo alishindwa kutaja majina ya majeruhi
kutokana na baadhi yao kuendelea kupatiwa matibabu kwa ajili ya kuokoa maisha
yao.
Naye Mganga wa Hospitali ya Mtakatifu Kizito iliyopo Mikumi, Dk
Boniventure Buyagabuyaga, alithibitisha kupokea jumla ya miili ya marehemu 18
ambao walikuwa wameteketea vibaya kwa moto kutokana na ajali, ambapo alisema
tayari imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhiwa maiti kwa ajili ya kusubiri
utambuzi.
Alisema mpaka sasa majeruhi wanaotibiwa katika hospitali yake
wamebaki saba, lakini hali zao bado ni mbaya kutokana na kuungua moto katika
sehemu mbalimbali za miili yao.
Ajali hiyo imekuwa sawa na mwendelezo wa ajali za mabasi nchini,
kwani Alhamisi iliyopita watu 12 walikufa katika ajali zilizotokea Tanga na
Morogoro, huku wengine wanne waliokuwa wakisafiri kwa basi la Nyehunge wakiaga
dunia usiku wa Jumamosi mkoani Dodoma.
Katika ajali iliyotokea mkoani Tanga, katika kijiji cha Mbweni
Mkata, majira ya asubuhi, ilihusisha basi la Kampuni ya Ratco ya Tanga
liligongana uso kwa uso na basi la kampuni ya Ngorika na gari dogo aina ya
Toyota Passo na kusababisha vifo vya watu 10 papo hapo, akiwemo mmiliki wa gari
dogo, Musa Lupatu aliyekuwa Mbunge wa zamani wa Korogwe Vijijini.
Katika tukio la Morogoro, watu wawili walikufa na wengine 48
kujeruhiwa katika ajali iliyosababishwa na basi la Happy Nation lililokuwa
likitoka Dar es Salaam kwenda Mbeya na kupata ajali eneo la Mikumi.
Aidha, Machi 12, mwaka huu mkoani Iringa, basi la Majinja Express
lilikuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam liligongana na lori na kisha
likaangukiwa na kontena lililosababisha vifo vya watu 43.