Saturday, 18 April 2015

AUNT AMWAGA MACHOZI KULAANIWA KIFO


MWIGIZAJI ‘mama kijacho’ Aunt Ezekiel amejikuta akidondosha machozi ya uchungu baada ya shabiki mmoja kujitokeza kwenye mtandao wa kijamii na kumlaani kifo.

Tukio hilo lilitokea juzikati baada ya Aunt kuweka picha iliyomuonyesha akiwa na Wema kwenye mtandao wa Instagram akiwa ameshika tumbo lake ndipo mfuasi wa mtandao huo anayetumia jina la Said Ulimwengu alipoibuka na ‘kukomenti’ kuwa mtoto atakayezaliwa atakuwa amelaaniwa na hata akijifungua afe na kiumbe chake.

Ujumbe huo ulisomeka hivi: “Yani ukijifungua naomba ufe na mimba yako maana utakachokizaa kimeshalaaniwa.”

Chanzo makini kimeeleza kuwa, kitendo cha shabiki huyo kuandika maneno hayo mtandaoni kilimkwaza sana Aunt na kujikuta akibubujikwa na machozi sambamba na kushukwa na presha lakini bahati nzuri alikunywa dawa za kuipandisha, akarejea katika hali yake ya kawaida.

“Ilikuwa hatari kweli, presha ilishuka sana lakini bahati nzuri alikuwa na dawa za kupandisha akanywa ndiyo akakaa sawa,” kilisema chanzo chetu.

Aunt alipotafutwa kuhusiana na habari hiyo alikiri kutokea na kudai amejisikia vibaya sana shabiki huyo pamoja na mashabiki wengine kupenda kujadili tumbo lake. 

“Najua ni wengi wanatamani kuniona sipo lakini kila kitu ni Mungu atapanga na si binadamu yeyote hapa chini ya jua,” alisema Aunt.