Wednesday, 11 March 2015
ZEC: Kura ya maoni ipo pale pale
TUME ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imesema haina sababu ya kusitisha zoezi la upigaji wa kura ya maoni juu ya katiba inayopendekezwa. Mtaalamu wa sheria katika tume hiyo, Khamis Issa Khamis, aliyasema hayo wakati akitoa ufafanuzi juu ya hoja inayotolewa na baadhi ya wanasheria kwamba Zanzibar haitaweza kupiga kura ya maoni kwa vile sheria iliyotumika kuunda Bunge la Katiba, haikuridhiwa na Baraza la Wawakilishi.
Alisema madai hayo hayana ukweli, kwa vile kifungu cha 64 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeeleza wazi masharti yanayoipa haki Zanzibar ya kuendesha zoezi hilo. Alisema ni kweli wamezisikia hoja zinazotolewa na baadhi ya wanasheria hao, lakini bado kinachoonekana wameshindwa kuiangalia vizuri katiba hiyo.
Akifafanua kauli yake hiyo, alisema kwa mujibu wa kifungu cha 64, kinachosimamia madaraka ya kutunga sheria, kifungu kidogo cha (1) kimeeleza kwamba mamlaka yote ya kutunga sheria juu ya mambo mengine yote yanayohusuyoTanzania Bara, yatakuwa mikononi mwa Bunge, huku kifungu kidogo cha (2), kikieleza kuwa Mamlaka yoyote ya kutunga sheria katika Tanzania Zanzibar, juu ya mambo yote yasio ya Muungano yatakuwa mikononi mwa Baraza la Wawakilishi.
Alisema, katika kifungu kidogo cha (3), kinafahamisha endapo sheria yoyote iliyotungwana Baraza la Wawakilishi, inahusu jambo lolote katika Tanzania Zanzibar, ambalo liko chini ya mamlaka ya bunge sheria hiyo itakuwa ni batili, na itatambulika na pia endapo sheria yoyote iliyotungwa na Bunge inahusu jambo lolote ambalo liko chini ya Mamlaka ya Baraza la Wawakilishi, sheria hiyo itakuwa ni batili na itatenguka.
Mwanasheria huyo, pia alisema katika suala hilo bado kifungu kidogo cha 64 (4) kinaeleza kuwa, sheria yoyote iliyotungwa na Bunge kuhusu jambo lolote, haitatumika Tanzania Zanzibar, ila kwa mujibu wa masharti yalioainishwa ndani ya Katiba hiyo.
Akitaja masharti hayo, alisema, katika kifungu kidogo cha (4) kipengele (a), kinaeleza sheria hiyo iwe imetamka wazi kwamba itatumika Tanzania bara na vile vile Tanzania Zanzibar, au iwe inabadilisha, kurekebisha, au kufuta sheria inayotoka Tanzania Zanzibar.
Kifungu (b), alieleza mtaalamu huyo, alisema, kinaeleza kuwa sheria hiyo, iwe inabadilisha au kurekebisha au kufuta sheria iliyokuwa inatumika tangu zamani Tanzania Bara, ambayo pia ilikuwa inatumika pia Tanzania Zanzibar, kwa mujibu wa mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ya mwaka 1964 au kwa mujibu wa sheria yoyote ambayo ilitamka wazi kwamba itatumika Tanzania Bara na vile vile Tanzania Zanzibar.
Aidha, haki hiyo, alisema pia imeoneshwa katika kifungu kidogo cha © ndani ya katiba hiyo, kinachoeleza kwamba sheria hiyo iwe inahusu mambo ya Muungano na kila inapotajwa Tanzania katika sheria yoyote ifahamike kuwa sheria hiyo itatumika katika Jamhuri ya Muungano kwa mujimu wa ufafanuzi uliotolewa na ibara hiyo.
Alisema kura ya maoni itafanyika kama ilivyopangwa na hawaoni sababu ya kuahirisha zoezi hilo, kwa vile bado hakujawa na sababu za msingi.
Akizungumzia juu ya suala la asasi za kiraia ambazo zinatarajiwa kushiriki katika uchaguzi huo, alisema hadi sasa kwa upande wa Zanzibar zilizoomba ni 135 huku kwa upande wa Tanzania Bara zimefikia asasi 375.