Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi
akizungumza na Wananchi wa Mtambwe baada kutembelea bara bara za ndani
zinazojengwa kwa msaada wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo ( IFAD ).
Balozi Seif akawataka
kushirikiana na wawekezaji walioamuwa kuweka miradi yao ya kiuchumi katika
maeneo yao ili nao wapate ajira na kuongeza kipatyo chao cha kila siku.
Afisa Mdhamini Wizara ya Miundo
Mbinu na Mawasiliano Pemba Nd. Hamad Ahmed Baucha akimpatia maelezo Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif kuhusu ujenzi wa Bara bara ya Ole- Kengeja
inayogharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Kulia ya Balozi Seif ni Mhandisi
Muelekezi wa ujenzi wa Bara abara hiyo Ndugu Remidius Edington Kisasi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema
kwamba dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuharakisha miundo mbinu ya
Mawasiliano ya Bara bara ili kuwapa fursa nzuri Wananchi wake kupata
huduma zilizo bora za usafiri.
Balozi Seif alisema hayo wakati akizungumza na wananchi wa
Kijiji cha Mtabwe alipokuwa akizikaguwa Bara bara za ndani zinazojengwa na
msaada wa Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo { IFAD } chini
ya Usimamizi wa Wizara ya Kilimo na Mali Asili Zanzibar kupitia Mradi wa MIVARF
akiwa katika ziara ya siku mbili kukaguwa shughuli za Maendeleo Kisiwani Pemba.
Alisema Serikali mbali ya kuendelea kuweka miundo mbinu ya
Bara bara Kuu lakini pia imeazimia kuzitengeneza bara bara za
Vijijini pamoja na Mashambani kwa lengo la kuweka uwiano wa upataji wa huduma
za usafiri kwa wananchi wa maene yote Nchini.
Balozi Seif alieleza kwamba huduma muhimu na za lazima kwa
wananchi zitaendelea kusambazwa na Serikali ikiwa ni itekelezaji wa Ilani ya
chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2010 iliyonadiwa na kupata ridhaa ya wananchi
walio wengi Nchini.
Akigusia sekta ya uwekezaji Makamu wa Pili wa Rais wa
Zanzibar aliwaomba wananchi waendelee kushirikiana na
wawekezaji katika miradi wanayowekeza nchini ambayo husaidia kutoa
ajira hasa kwa Vijana.
Alifahamisha kwamba Safari za Viongozi wakuu wa Kitaifa
wakiwemo Mawaziri wa Wizara tofauti Nchini huzitumia katika kushawishi
mashirika na makampuni kuja kuwekeza miradi hyao nchini kwa lengo la kuunga
mkono uimarishaji wa Mapato ya Taifa.
Balozi Seif aliwatahadharisha wananchi wa Kisiwa kidogo cha
Uvinje kiliopo Kaskazini ya Pemba kwamba hawana haki ya kukataa miradi
iliyoamuliwa na Serikali kuwekezwa Kisiwani humo.
Alieleza kwamba hakuna Kikundi au Mtu anayeweza kuchukuwa
hatua za kupinga maamuzi yanayotolewa na Serikali katika matumizi ya
ardhi ambayo ni mali ya Serikali kwa mujibu wa Sheria zilizopo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka wananchi hao
washirikiane na mwekezaji aliyepewa fursa na Serikali kuwekeza Kisiwani humo na
si busara kuisubiri Serikali Kuu itumie nguvu.
Mapema Kaimu Afisa Mdhamini Wizara ya Kilimo na
Mali Asili Pemba Nd. Mbarouk Ali Mgau alimueleza Balozi Seif kwamba Ujenzi wa
Bara bara za ndani Kisiwani Pemba zenye urefu wa Kilomita 80 kwa kiwango cha
kifusi utakaogharimu jumla ya shilingi Bilioni 6.4 unaendelea vyema.
Nd. Mbarouk alisema ujenzi huo Unaosimamiwa na Wizara ya
Kilimo na Mali Asili Zanzibar umefadhiliwa na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo
ya Kilimo { IFAD }, Benki ya Maendeleo ya Afrika { ADB } kwa kushirikiana na
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Alisema zipo baadhi ya changamoto zinazosababisha vikwazo
vya ujenzi wa Bara bara hizo akizitaja kuwa ni pamoja na umuhimu wa ushirikiano
kati ya taasisi husika na wananchi katika kuzitunza bara bara hizo.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkaazi wa Mamlaka ya Uwekezaji Vitega
Uchumi Pemba { ZIPA } Nd.Ali Shaaban Suleiman alisema Mkoa wa Kaskazini Pemba
bado uko nyuma katika uwekezaji vitega uchumi.
Nd. Shaaban alisema uchelewaji wa uwekezaji miradi ya
Kiuchumi ndani ya Mkoa huo hasa katika Sekta ya Utalii unaviza kutokana na
baadhi ya wananchi wa mkoa huo kushutumu kwamba utalii umekuwa ukiharibu mila
na silka za Wananchi hao.
Aliutaja Mradi wa uwekezaji ambao tayari umeshapata kibali
kutoka Taasisi husika za Serikali ni ule wa Oxgen Holding Company wenye mtaji
wa Dola za Kimarekani Milioni Tano utakaohusisha nyumba za kulala wageni pamoja
na michezo mbali mbali ya Baharini.
Alisema mradi huo licha ya kupata vikwazo katika Kisiwa cha
Uvinje lakini umelenga kutoa huduma za Maendeleo ya Wananachi pamoja na zile za
kijamii na kuliongezea mapato Taifa.
Katika ziara hiyo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi
Seif Ali Iddi alipata fursa ya kuzitembelea bara bara za ndani kIsiwani Pemba
za Mchangamdogo/Kinyikani hadi Mzambarauni, Bara bara ya Mkanjuni/ Kivumoni
pamoja na ile ya Ole Kengeja inayogharamiwa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.