Monday, 25 May 2015

MSUMBIJI YAITOA MALAWI KOMBE LA COSAFA

MSUMBIJI imeitoa Malawi katika Kombe la COSAFA kwa ushindi wa penalti 5-4 baada ya sare ya 2-2 Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace mjini Rusternburg, Afrika Kusini usiku wa leo.

Msumbiji walikuwa na bahati ya aina yake leo, kwani mabao yao yote wapinzani walijifunga, kwanza Malata dakika ya 10 na baadaye Mzava dakika ya 90.

Mabao ya Malawi ambao leo walicheza nyuma ya bahati, yalifungwa na Sulumba dakika ya 51 na Mzava kwa penalti dakika ya 90.

Malawi sasa itacheza na Afrika Kusini Jumatano katika Nusu Fainali ya vibonde, maarufu kama michuano ya Plate Uwanja wa Bafokeng, kuanzia Saa 1:00 usiku, mchezo utakaotanguliwa na Nusu Fainali nyingine ya Plate kati ya Zambia na Ghana Saa 11:00 jioni.

Mapema jioni ya leo, Madagascar waliitoa Ghana baada ya kuichapa mabao 2-1 katika Robo Fainali ya tatu Uwanja wa Royal Bafukeng Sports Palace.

Juzi, Namibia iliwatoa mabingwa watetezi Zambia kwa penalti 5-4 baada ya sare ya 0-0, wakati Botswana iliwatoa wenyeji Afrika Kusini kwa penalti 7-6 baada ya sare ya bila mabao pia.

Msumbiji inaungana na Madagascar, Botwsana na Namibia katika mbio za Kombe la COSAFA 2015.