Vyombo vya usalama nchini Kenya, vinawashikilia
wasichana watatu akiwamo Mtanzania, kwa kile kunachodaiwa kutaka kujiunga na
kundi la kigaidi la al-Shabaab huko Somalia.
Taarifa
kutoka kwa Kamishna wa Polisi Jimbo la El -Wak, mpakani mwa Kenya na Somalia,
Nelson Marwa amesema Mtanzania aliyekamatwa, alijieleza kuwa ni mwanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Afrika, Sudan.
Mtanzania
huyo, Ummul-Khayr Sadir Abdul (19), mwenyeji wa Zanzibar, anatajwa kuwa
kiongozi wa kundi hilo lililopanga kujiunga na al-Shabaab.
Wasichana
wengine waliokamatwa pamoja na Ummul-Khayr, ni Maryam Said Aboud na Khadija
Abubakar Abdulkadir wote raia wa Kenya.
“Hawa
wasichana watatu, inaaminika kuwa walikuwa wanakwenda Somalia kupata mafunzo ya
kigaidi na baadaye kufanya mashambulizi ya kujitoa mhanga,” alisema Kamishna
Marwa.
Akizungumzia
suala hilo, Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai, DCI Diwani Athumani alisema:
“Tunafuatilia hatujapokea taarifa zaidi ya hizo.”
Kamishna
Marwa alisema raia hao wawili wa Kenya, mmoja ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha
Mount Kenya kilichopo Thika, Jimbo Kiambu na mwingine ni mwanafunzi wa
Sekondari ya Burhania, iliyopo Malindi, Kilifi.
“Serikali
imepata taarifa kuhusu watu wanaokusanya watu kutoka Afrika Mashariki ili
wakajiunge na makundi ya ugaidi nchini Somalia, wakala wetu wa usalama wamepata
taarifa hizo na kufanikisha kukamatwa kwa wasichana hao,” alisema Kamishana
Marwa.
Hivi
karibuni, tovuti ya al-Jazeera ilitoa taarifa za kukamatwa kwa mkanda wa video
ulioonyesha mwakilishi wa kundi la kigaidi la Dola ya Kiislamu ya Iraq na
Levant (ISIL) akimtaka kiongozi wa kundi la al-Shabaab kuliimarisha kwa kufanya
mashambulizi ya kigaidi katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam.
Kamishna
Marwa alisema ingawa nyaraka za wasichana hao zote zinaonyesha kuwa ni
wanafunzi, lakini bado walibanwa kwa maswali kuhusu sababu inayowapeleka nchini
Somalia.
Aliongeza
zaidi kuwa chanzo cha habari cha kiusalama kilieleza kuwa nyaraka za wasichana
hao zilionyesha kuwa walikuwa wakienda kuolewa na wanajeshi wa kundi la
al-Shabaab.
Credit:BBC