Tuesday, 31 March 2015

Maalim Seif ahudhuria mazishi ya mwanachama wa CUF na kuwazuru majeruhi

Katibu Mkuu wa CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amehudhuria mazishi ya Hemed Salum Hemed (38) aliyefariki katika ajali ya barabarani iliyotokea wakati akirudi katika mkutano wa hadhara wa chama hicho uliofanyika Makunduchi Wilaya ya Kusini Unguja.
Marehemu ambaye ni mkaazi wa Kinuni, Wilaya ya Magharibi Unguja amesaliwa katika Msikiti Ngamia, Kilimahewa na kuzikwa Kianga, mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.
Aidha, Maalim Seif amewatembelea na kuwafariji baadhi ya wafuasi wa chama hicho waliojeruhiwa na watu wasiojuilikana wakati walipokuwa wakirudi katika mkutano huo walipofika eneo la Fuoni. Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Haki za Binadamu wa CUF bibi Pavu Juma, katika tukio hilo vijana waliokuwa katika gari eneo la Fuoni Taveta wakiwa na mapanga, nondo na mawe walianza kuwarushia mawe wafuasi wa CUF waliokuwa kwenye magari wakitokea katika mkutano Makunduchi na kuwajeruhi wafuasi 24 wa chama hicho.
Amesema baadhi ya majeruhi hao wamepata majeraha makubwa na wamelazwa katika hospitali ya Mnazimmoja, na wengine wamesafirishwa hadi Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.
Mapema akiwatembelea baadhi ya majeruhi huko Mwembemakumbi, Katibu Mkuu huyo wa CUF, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema watu waliowajeruhi wafuasi wa CUF wamefanya hivyo baada ya chama chao kukosa Sera za kuwaeleza Wananchi na sasa wameamua kufanya hujuma ambazo amesema hazitowasaidia. Amerejea wito wake wa kuwataka wanachama na wafuasi wa CUF wawe watulivu na kwamba chama hicho kinafuatilia kwa karibu hujuma zote zinazofanywa dhidi yao.