Kwa sasa tunapozungumzia mastaa wa muziki wanaofanya vizuri hapa Bongo,
jina la Nasibu Abdul ‘Diamond’ lazima litachukua nafasi ya kwanza kisha wengine
watafuata. Ni kijana anayejituma sana na jitihada zake hizo zimemfanya awe
maarufu barani Afrika.
Picha tofauti wakati wa utoto wao.
Nyuma ya
mafanikio ya Diamond wapo watu wengi. Mwenyewe amekuwa akimshukuru sana mama
yake, Sanura Kassim ‘Sandra’ kwa malezi aliyompa hadi kufikia hapo alipo leo.
Ukimuacha mama yake, wapo watu wengine wengi lakini leo nataka kukupa angalau
kwa uchache uhusiano uliopo kati ya Diamond na DJ wake, Romy Jones.
Katika
safari ya kimuziki, Diamond na Romy wametoka mbali sana. Kwa wasiojua, wawili
hawa ni ndugu kabisa, ni mtu na kaka yake kwa upande wa mama zao. Yaani mama wa
Diamond na mama wa Romy ni mtu na dada yake.
Mwandishi
wa makala haya, alipata nafasi ya kuzungumza na Diamond juu maisha yake na Romy
enzi za utoto wao, soma hapa chini…
Maisha ya
utotoni
Diamond:
“Awali Romy alikuwa akiishi Kinondoni kwa baba yake lakini kila wikiendi
alikuwa anakuja Tandale, tunakula ‘good time’ kisha anaondoka. Ikafika kipindi
baba yake akafariki na hapo ndipo mama wa Romy alipolazimika kurudi kwao,
Tandale akamkuta dada yake (mama Diamond) akiwa na mimi. Hapo ndipo tukakua na
kucheza pamoja.
“Hakuna
sehemu ambayo ungemkuta Romy bila mimi kuwepo. Yalikuwa ni maisha f’ulani
ambayo natamani yajirudie. “Ukweli Romy alikuwa ni mkubwa kwangu lakini
tuliishi kama mapacha licha ya kwamba Romy alikuwa mtundu kuliko mimi.
Nasibu Abdul ‘Diamond’.
Ishu ya shule ikawaje?
Kwa namna tulivyokuwa ilikuwa ngumu kupelekwa shule tofauti, tulisoma
shule moja kuanzia shule ya msingi hadi sekondari.
Ubishoo ilikuwa tangu utotoni
“Unajua sisi wazazi wetu walikuwa wa kisasa, walikuwa wanajua
kutuvalisha vizuri na ndiyo maana picha nyingi za utotoni cheni, raba, jinzi na
tisheti za kijanja kama kawa. Kwa hiyo huu usafi hatukuuanzia juzi wala jana,
sisi tangu ‘long time’ kitambo.”
Walichopendelea zaidi
“Enzi hizo tukiwa wadogo hatukujua kama tutakuja kufanya muziki,
tulifanya mambo mengi ya kitoto tu. Tulikuwa tunacheza sana mpira kama ilivyo
kwa watoto wengine.”
Muziki ilikuwaje?
“Wakati tuko wadogo, nakumbuka kuanzia tukiwa shule ya msingi, mama
yangu alikuwa akitupeleka sana kwenye maeneo ya burudani. Ikitokea kuna
mashindano ya kuimba ‘talent show’ alikuwa akitushika mkono na kutupeleka, huko
ndiko tulikoanzia mambo ya muziki.”
Mwanzo wa ustaa
Romy Jones.
Romy alipokuwa akifanyiwa ‘intaviu’ katika Kipindi cha Sporah hivi
karibuni alisema: “ Wakati nilipoanza kufanya kazi ya utangazaji pale Clouds,
Diamond hakuwa lolote, alikuwa akiniona kwenye TV, yeye bado anapambana na
maisha ya uswahilini huku akifanya muziki.
“Wakati mimi naanza kupata zile elfu 10 na zaidi, yeye alikuwa hana
hata mia. Nikawa namtoa kimtindo.
“Ikafika kipindi ndiyo nikamtambulisha Diamond kwa watangazaji wenzangu
akiwemo Adam Mchomvu, nikawaambia nina mdogo wangu anaitwa Diamond anaimba,
tunamsaidiaje.
“Tukarekodi nyimbo kibao zikaishia hewani. Kuna moja ya kurap tukafanya
na Gez Mabovu na NGwea (wote marehemu) kisha nikaipeleka Clouds. Mchomvu
alipoisikia akaipenda ikaanza kupigwa, Diamond akawa anafurahi sana. Safari ya
kimuziki ikaanzia hapo na mpaka sasa mimi ni Official DJ na Tour Manager wa
Diamond