PAMOJA na mwenyewe
kukanusha kuwa si mtumiaji wa madawa ya kulevya (unga), watu wanazidi kusema
eti supastaa wa sinema za Kibongo, Wema Sepetu ‘Madam’ anatumia unga, Risasi
Jumamosi limesheheni data.
UBUYU WAVUJISHWA
Kwa mujibu wa chanzo makini, Wema amekuwa akitumia kilevi hicho kwa muda mrefu
huku akifanya jambo hilo kwa siri kubwa.“Hivi hamna habari ya Wema kubwia unga?
Mbona kila mtu anajua, watu wengi tu wanafahamu lakini wanashindwa namna tu ya
kumueleza mwenyewe ili aache maana kila mtu anamhofia si unamjua naye Madam mtu
wa kumaindimaindi,” kilisema chanzo hicho.
MITANDAO YAKAZIA MADAI
Kama hiyo haitoshi, kwa nyakati tofauti, watumiaji mbalimbali wa mitandao ya
kijamii wamekuwa wakidai kuwa staa huyo anabwia unga licha ya kuwa hawana
ushahidi wa moja kwa moja.“Mimi sijawahi kumuona lakini kuna watu wake wa
karibu tu wananihakikishia kwamba Wema anatumia madawa ya kulevya, ila naamini
mwenyewe anaujua ukweli wote wa haya yanayosemwa,” ilisomeka sehemu ya maoni
mtandaoni.
RISASI LAMFUNGIA KAZI
Baada ya kupata madai hayo, Risasi Jumamosi lilimfungia kazi Madam ili kuweza
kumsikia anazungumziaje tuhuma hizo nzito.
Jumatano iliyopita,
mwanahabari wetu alikwenda nyumbani kwa mwigizaji huyo mwenye mvuto wa kipekee,
Mtaa wa Bwawani-Kijitonyama lakini bahati mbaya alikuwa ametoka kwenda kurekodi
na hata alipofanya subira hadi jioni, bado hakurejea huku simu yake ikiita bila
kupokelewa.
JITIHADA ZAIDI
Siku iliyofuata, mwanahabari wetu aliyeambatana na mmoja wa wahariri wa Global
Publishers, walitia timu kwa mara nyingine nyumbani kwa Madam lakini pia
mwigizaji huyo alikuwa ametoka lakini bahati nzuri alipopigiwa simu alipokea,
mambo yalikuwa hivi:Risasi: Wema tumekutafuta sana hapa nyumbani kwako bila
mafanikio tuna ishu ya msingi kweli tunataka kujua kutoka kwako?
Wema: Poleni, ishu gani?
Risasi: Tumepokea habari kuwa wewe unatumia madawa ya kulevya, umewahi
kusikia hizi habari?
Wema: Ndiyo hizo habari nimewahi kuzisikia. Nakumbuka nilianza kuzisikia tangu
kipindi kile mimi natembea na CK (yule kigogo wake), walivumisha sana lakini
hakuna ukweli wowote.
ADAI WAMEMPONZA
“Tena imefika wakati wananikosesha hadi amani, imenifanya hadi niwe nakaguliwa
kupindukia bila sababu za msingi, juzi hapa wakati naenda Mwanza (kwenye shoo
ya Instagram), walinibana sana pale Air Port hadi nikataka kuachwa na ndege.
AISHI KWA TAHADHARI
“Yaani kwa sasa nimelazimika kuweka hadi ulinzi mkali pale nyumbani, maana
huwezi jua watu wasionipenda wanaweza kuja wakanibambikia nikaonekana natumia
kumbe sijui hata ukoje. Sasa hivi kila atakayeingia lazima akaguliwe, ahojiwe
ndipo aingie.
ATAJA KUHUSISHWA NA ROMMY
“Kuna wakati walinitaja kuwa natumia kwa kuwa nina ukaribu na Rommy Johnson
(binamu yake msanii Diamond) kitu ambacho nilikikanusha na ninaendelea kusema
hakuna ukweli wowote.
MAMA’KE ARIPOTI POLISI
“Ili kuwataka watu wasinihusishe kwa namna yoyote na kujihadhari, tuliongea na
mama, akaenda kutoa taarifa polisi Mabatini ili nisije kupata tatizo lolote
linalohusishwa na madawa ya kulevya.”
RAFIKI ZAKE WANENA
Mwanahabari wetu aliwavutia waya marafiki wa Wema, Aunt Ezekiel na Martin
Kadinda ambaye ni meneja wa mwigizaji huyo ambao kwa pamoja walidai hawajawahi
kumuona Madam hata siku moja akibwia unga achilia mbali kukaa karibu na
wabwiaji.
“Sijawahi kumuona Wema
hata siku moja anatumia hivyo vitu (unga), watakuwa wanamzushia ili watimize
azma yao ya kumchafua si unajua si wote wanampenda?,” alisema Aunt huku Martin
akikazia:“Hakuna kitu kama hicho, Madam hatumii bwana, sisi tupo naye,
tunafanya naye kazi siku zote, hatujawahi kumuona, huo ni uzushi tu.”
credit:GPL