Wednesday, 20 May 2015

VURUGU ZAZUKA NJOMBE BAADA YA POLISI KUDAIWA KUUA

Wakazi mkoa wa Njombe wameandamana baada ya polisi kudaiwa kumuua raia mmoja kwa kumpiga risasi na kujeruhi mwingine kadhaa katika Mtaa wa Kambarage.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Ambaye ni Afisa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Njombe Franco Kibona.

Aliyeuawa katika tukio hilo ni Basil Ngole mkazi wa Mtaa wa Kambarage na aliyejeruhiwa ni Fred Sanga mkazi wa mtaa huo ambapo kwa sasa amelazwa katika hospitali hiyo.

Kufuatia tukio hilo wananchi walikusanyika hospitalini hapo kupinga polisi kuua, na kulitaka jeshi la polisi kugharamia mazishi ya marehemu pamoja na matibabu ya aliyejeruhiwa.

Kutokana na hali hiyo polisi walifika eneo la tukio na kuanza kuwatawanya waandamanaji hao kwa mabomu ya machozi na kupelekea mwananchi mmoja kujeruhiwa aliyejulikana kwa jina moja la Mandele.

Wakizungumzi tukio hilo baadhi wa wananchi mjini hapa, walilaani kitendo cha polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia wasiokuwa na hatia, huku wakiomba askari aliyetekeleza mauaji hayo na majeruhi kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Emanuel Filangali mkazi wa Njombe alisema hata kama marehemu na majeruhi na raia wengine walikuwa na kosa la kunywa pombe nje ya muda katika klabu hicho walipaswa kukamatwa na siyo sakari kuwapiga risasi na kusababisha kifo pamoja na majeruhi.

Kwa upande wake diwani wa kata ya Njombe Mjini Agrey Mtambo alisema askari walifika katika klabu hiyo ambapo waliwakuta watu wakiwa wanakunywa pombe ambapo waliwaamuru kukaa chini

Aliongeza kuwa licha ya jeshi la polisi kufanya makosa ya kumuua mwananchi bado wameendelea kuwatanya wananchi kwa mabomu ili hali wanajua kwamba wapo katika taharuki hivyo kuitaka serikali kuwajibika kwa kushughulikia matatizo ya wananchi ili kuondoa adha zinazowakabili wananchi.

Katika hali nyingine vurugu hizo za wananchi zilizokuwa zikizuiliwa na askari polisi zimesababisha kusimama kwa shughuli nyingi mjini hapa hususani biashara ambapo watu walilazimika kufunga maduka ili kupisha mzozo huo ambao ulizua tafrani kwa wananchi walio wengi.