STAA mkongwe wa
sinema za Kibongo, Ruth Suka ‘Mainda’ ametoa ushuhuda mzito (confession) baada
ya kukiri kuishi maisha ya starehe ikiwemo unywaji pombe na kukosea mwanaume
sahihi wa maisha kwa kuingia kwenye uhusiano tofauti jambo aliloliita ni
‘kumtumikia shetani kwa pombe na ngono’.
Akizungumza kwa njia ya
simu na mwandishi wetu hivi karibuni katika mahojiano maalum, Mainda ambaye kwa
sasa ni mlokole wa ‘tuimbe na kusifu’ aliweka wazi kuwa kipindi cha nyuma,
shetani alimzidi nguvu kwa kujichanganya maeneo ya baa na kunywa pombe jambo
ambalo kwa sasa kila akikumbuka huishia kusikitika.
Alisema, kwa sasa hana
mpenzi na kwamba hatafuti lakini anamngojea yule ambaye anaamini atatoka kwa
Mungu kwa wakati muafaka.Mainda aliweka wazi kuwa anamshukuru Mungu kwa
kumuongoza katika njia nyoofu huku akiainisha kuwa maisha bila ya kuwa na Mungu
ni ya ajabu sana.
“Kwa kweli maisha ya
zamani yalikuwa ya ajabu, ulevi wa pombe, kutoka na wanaume tofauti nikidhani
ndiye mwanaume sahihi, zilikuwa ni nguvu za shetani, namshukuru Mungu kwa
kunibadilisha kwa kiwango hiki kwani nilimtumikia sana ibilisi kwa mambo
machafu, viongozi wangu wa dini wananipa mwanga mkubwa mno juu ya Neno la Mungu
na kila nikikumbuka maisha ya nyuma, huwa siyatamani kabisa,” alisema Mainda.