Friday, 8 May 2015

Lulu Michael: SINA JINI MAUTI


MSANII nyota wa filamu, Elizabeth Michael `Lulu' amekanusha uvumi kuwa matatizo yanayowatokea wanaume aliowahi kuwa nao yanatokana na yeye kuwa na Jini Mauti anayesababisha hali hiyo kutokea, Amani linakujuza.

Akizungumza na Gpl juu ya madai ya wadau mbalimbali kuhusiana na matukio mengi yanayomtokea, muigizaji huyo wa filamu ya Foolish Age, alisema maisha yake ya siku hizi ni ya kusali sana, hivyo anaamini kutokana na maombi yake, hali yake iko vizuri kutokana na Mungu kumpa anachokihitaji.

"Ninasali sana kwa sasa aisee, mara nyingi nafanya hivyo mara tatu kwa siku, ninao uwezo wa kukemea mapepo na yakaondoka, hayawezi kukaa mwilini mwangu," alisema muigizaji huyo ambaye miaka michache iliyopita, aliondokewa na mpenzi wake, Steven Kanumba aliyeanguka na kufariki mbele yake.

Mtabiri mmoja maarufu jijini Dar es Salaam, Maalim Hassan Yahya Hussein, alisema tatizo kubwa linalomsumbua binti huyo ni jini mauti ambalo baada ya kumpenda, halitaki kuridhia uhusiano wake wa kimapenzi na binadamu.

"Hapa nimshauri tu, achukue hatua ya matibabu haraka iwezekanavyo vinginevyo hali hiyo itaendelea, anatakiwa afanye kafara kwa kuchinja mnyama yoyote ili aondokane na matatizo haya," alisema.