Safari ya mbunge wa zamani
wa Kigoma Kaskazini kwa tiketi ya Chadema, Zitto Kabwe kurejea bungeni imeanza
rasmi baada ya kiongozi huyo wa chama kipya cha ACT-Wazalendo kuchukua fomu za
kuwania kuongoza jimbo la Kigoma Mjini.
Uamuzi huo wa kulitaka jimbo hilo unathibitisha kauli zake ambazo amekuwa
akizitoa kwa muda mrefu kuwa hatarudi tena Kigoma Kaskazini kwa kuwa
alishawatimizia kila kitu na haoni sababu za kuwawakilisha tena wananchi wa
eneo hilo.Kauli yake iliibua ubashiri kuwa Zitto anataka kubadilishana jimbo na mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, uvumi ambao aliukanusha akisema hadhani kama CCM inaweza kupata jimbo Kigoma.
Zitto, ambaye alijiondoa Chadema baada ya kukiuka katiba kwa kufungua mashtaka dhidi ya chama hicho, hakufanya mbwembwe wakati akienda kuchukua fomu kwenye ofisi za ACT Ujiji jana, badala yake aliita viongozi wa kata na matawi bila ya kutaarifu vyombo vya habari.
“Nimeamua kugombea ubunge wa Kigoma Mjini ili niwatumikie ndugu zangu ambao wamekuwa wakipata tabu katika kupigania haki zao za msingi ambazo walistahili kuzipata kama ilivyo katika mikoa mingine,” alisema Zitto alipoongea na mwandishi wa Mwananchi kwa simu.
“Nitakapokuwa mbunge wa Kigoma Mjini nitahakikisha barabara za mitaani zinapitika katika kipindi chote cha mwaka, nitahakikisha watu wanaacha tabia ya kulima mashamba katikati ya mitaa na makazi, lakini nitahakikisha kila mmoja anajiunga na mifuko ya kijamii ili kujiwekea akiba ya uzeeni pamoja na kupata huduma ya matibabu, elimu na nyinginezo zinazopatikana kwa kutumia mifuko hiyo.”
Mwenyekiti huyo wa zamani wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema bonde la Mto Luiche bado halijatumika ipasavyo kuzalisha chakula kwa wingi.
“Nakusudia kuibana Serikali ijenge skimu ya umwagiliaji maji ili wakulima walime kilimo cha mpunga kwa mwaka mzima bila kupumzika, jambo ambalo litainua uchumi wa wakulima na kuongeza chakula hapa Kigoma,” alisema.
Kuhusu umeme wa gridi ya Taifa, Zitto alisema lazima upatikane ili kusaidia jitihada ya ujenzi wa viwanda vya kusindika mazao ya uvuvi na kilimo kwa kuwa hivi sasa mji wa Kigoma Ujiji unategemea umeme wa jenereta ambao hauwezi kuendesha shughuli za viwanda, hali inayochangia mkoa kuendelea kuwa masikini licha ya kuzungukwa na rasilimali nyingi.
Katibu wa ACT wa Jimbo la Kigoma Mjini, Azizi Ally alisema Zitto alichukua fomu hiyo jana kwa malipo ya Sh100,000 mbele ya viongozi 72 wa kata na matawi kutoka jimboni humo.
“Kwa hali ya sasa Kigoma Mjini inahitaji kupata mbunge anayeweza kufuatilia mambo kwa kina ili kuleta maendeleo ya wananchi baadala ya yule anayekwenda bungeni kujifunza,” alisema Ally.
“Watu wanakabiliwa na kero mbalimbali kama ubovu wa barabara za mitaani, uhaba wa umeme wa uhakika unaoweza kuendesha viwanda vikubwa na vidogo, pamoja na wengi kufanya kilimo cha kujikimu zaidi.“
Zitto alitofautiana na uongozi wa juu wa Chadema uliomtuhumu kuwa alikuwa amefanya uasi na kwamba alishaanzisha chama kingine akiwa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani na kusababisha avuliwe nyadhifa zote, ikiwamo ya unaibu katibu mkuu.
Hata hivyo, wakati Chadema ikijiandaa kumjadili na pengine kumvua uanachama, Zitto alifungua kesi akitaka mahakama imuamuru katibu mkuu wa Chadema ampe nyaraka za mwenendo wa vikao vilivyomvua madaraka na kuomba amri ya kuzuia vikao hivyo visimjadili.
Katika hukumu ya kesi hiyo, mahakama ilitupilia mbali hoja zake, uamuzi uliotafsiriwa kuwa umefungua njia ya kutimuliwa kwake kwa kitendo cha kufungua kesi mahakamani kinyume cha katiba.
Mkazi wa Gungu mjini Kigoma, Zuberi Mrisho alisema ujio za Zitto kugombea Ubunge wa jimbo hilo utaamsha ari ya wananchi kujiandikisha kwa wingi katika Daftari la Wapigakura na kujitokeza kupiga kura tofauti na chaguzi zilizopita.
“Mwaka 2010 Vijana wengi hatukupiga kura hapa kwa sababu tulikosa imani na baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali, lakini kwa ujio wa Zitto sasa nina hakika wengi tutajitokeza kupiga kura ili tupate viongozi makini kwa maslahi ya mji wetu,’ alisema Mrisho.