Kwa mujibu wa mkataba
huo, Iran itapunguza uwezo wake wa kurutubisha madini ya urani huku ikiahidiwa
kuondolewa vikwazo kwa awamu.
Rais Barack Obama
amesema ni "uelewano wa kihistoria" uliofikiwa na Iran.
Mataifa makubwa ya
dunia na Iran sasa yanalenga kuandika mkataba kabambe ifikapo Juni 30.
Muundo wa mkataba
ulitangazwa na Umoja wa Ulaya na Iran baada ya siku nane za majadiliano mjini
Lausanne.
Mazungumzo kati ya
mataifa makubwa matano jumlisha moja yaani-Marekani, Uingereza, Ufaransa, China
na Urusi pamoja na Ujerumani- na Iran katika mkutano uliofanyika mjini
Lausanne, uliendelea na kupitiliza muda uliopangwa wa kufikia tarehe 31 Machi.
Mwandishi wa BBC
kutoka mjini Lausanne, Barbara Plett Usher, anasema baada ya kupitiliza muda
uliopangwa na siku mbili za majadiliano ya kina kati ya Iran na mataifa sita
makubwa duniani wameelezea muundo wao uliofikiwa katika mkutano huo kama
mafanikio makubwa.
Mwanadiplomasia wa
ngazi ya juu wa Umoja wa Ulaya,Federica Mogherini, alisoma taarifa ya pamoja
ikielezea vipengele vikuu, ambavyo ni kupunguza vinu vya uchakataji wa fito za
nyuklia, kubadili zana za kutengenezea nyuklia na ahadi ya kuondolewa vikwazo
vya kimataifa dhidi ya Iran.
Makubaliano
yaliyofikiwa katika mkutano huo si ya maandishi, sio rasmi, bali yanajenga
msingi wa kufanyika mazungumzo ya kina.
Lakini waanzilishi wa
mazungumzo haya wanasherehekea mafanikio makubwa yaliyofikiwa, ambayo wanasema
ni ya kihistoria.
Iran imekuwa ikikana
madai ya mataifa ya magharibi kuwa mpango wake wa nyuklia unalenga kutengeneza
silaha za nyuklia. Iran imeingia katika mazungumzo haya ili kuona inaondolewa
vikwazo.
Katika mahojiano na
BBC, waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema ilifikia hatua
alishawishika kujitoa katika mazungumzo hayo lakini anasema cha msingi wameweza
kupenya vikwazo vilivyojitokeza katika awali.
Rasimu ya mazungumzo
hayo pia imepongezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ambaye
amesema anaamini "yatachangia hali ya amani na utulivu katika eneo
hilo".
Mkuu wa sera ya nje wa
Umoja wa Ulaya Federica Mogherini ametangaza mkataba huo katika mkutano na
waandishi wa habari akiwa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif,
akisema hiyo ni "hatua ya maamuzi" iliyofikiwa.
Urusi imepongeza
mkataba huo kuwa ni hatua ya kutambua mpango wa nyuklia wa Iran usio na
masharti na ambao ni salama.
Lakini kiongozi wa
Israel, Benjamin Netanyahu amemwaambia Rais Obama kwa njia ya simu kwamba
mkataba huo ambao umejikita katika muundo uliokubaliwa, unatishia uwepo wa
Israel.
Kwa upande wake Rais
Obama amemwambia Bwana Netanyahu kwamba mkataba huo kwa namna yoyote ile
unaondoa wasiwasi kwao kuwa Iran ni kinara wa kufadhili ugaidi na vitisho dhidi
ya Israel.
Mkataba huo pia
umekosolewa na wajumbe wa baraza la Congress la Marekani ambao wanataka wabunge
wa Marekani kuwa na haki ya kupitia kila makubalino ya mwisho yanayofikiwa
katika mkataba huo.
Nao wananchi wa Iran
wanaoishi nchini Uswisi wameelezea kufurahishwa na mpango huo.