Katika picha hii ya Maktaba,
Amiri Jeshi Mkuu , Rais Jakaya Mrisho Kikwete akimtunuku nishani ya kumbukumbu
ya miaka 50 ya Jeshi la Wananchi wa Tanzani ( JWTZ) Brigedia Jenerali Sara
Thomas Rwambali ambaye hivi karibuni, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa
Afrika, Dr. Nkosazana Dlamini Zuma amemteua
kuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Afrika nchi Sudani ya
Kusini.
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Dr. Nkosanzana
Dlamini Zuma, amemteua, Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali kutoka Jeshi la
Wananchi wa Tanzania ( JWTZ),kuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ofisi ya Umoja
wa Afrika Sudan ya Kusini .
Kwa
mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na AU na nakala yake
kutumwa Uwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, inaeleza
kwamba makazi ya Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali yatakuwa Juba.
Pamoja na
uteuzi wa Brigedia Jenerali Sara Rwambali, Dr. Nkosazana Dlamini Zuma pia
amewateua Madame Josephine- Charlotte Mayuma Kala kutoka Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo, anayekuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa
Afrika huko Cote d’Ivoire na makazi yake yakiwa Abidjan.
Wengine
walioteuliwa ni Madame Nyiramatama kutoka Rwanda, anayekuwa Mkuu wa Ofisi ya AU
huko Chad , makazi yake yakiwa Ndjamena na Dr. Arvin Boolel kutoka Mauritius
anayekuwa Mwakilishi Maalum na Mkuu wa Ofisi ya AU katika Maziwa Makuu Burundi
na makazi yake yakiwa Bujumbura.
Taarifa
kwa vyombo vya Habari kutoka AU inaeleza zaidi kwamba uteuzi huo ni sehemu ya
AU ya kuhakikisha uwepo wake katika kila eneo na vile vile kuunga mkono juhudi
zinazolenga katika kukuza Amani na Usalama Barani Afrika
“Ninatoa
pongezi zake za dhati kwa wateuliwa ambao ni viongozi wa ngazi za juu na wenye
sifa za kutukuka katika utumishi wa umma wakiwa na uzoefu mkubwa katika eneo la
amani na usalama. Si jambo la ajabu kwamba wateule watatu kati ya wanne ni
wanawake” anasema Dr. Zuma
Na
kuongeza, “katika mwaka huu wa 2015, ambao Umoja wa Afrika umejikita katika
uwezeshwaji wa wanawake. Ninayo matumaini makubwa kwamba AU na Afrika kwa
ujumla itanufaika na utaalamu na uzoefu mkubwa na uwezo wa kiuongozi kutoka kwa
wateuliwa hawa”.
Mwenyekiti
wa Kamishna ya AU pia ametoa wito kwa wadau wote kuwapatia ushirikiano
wateuliwa hao ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ukamilifu kwa maslahi ya
Bara la Afrika, huku akitoa shukrani kwa wawakilishi ambao wanamaliza muda wao.