Thursday, 16 April 2015
Ajali za Barabarani Zaua WATU 969 Ndani ya Siku 102 - Tanzania
WAKATI Rais Jakaya Kikwete akiungana na Watanzania kuomboleza vifo vya watu 19 walioteketea katika ajali ya basi lililoungua moto baada ya kugongana na lori juzi mjini Morogoro, imefahamika kuwa, ajali za barabarani zimegharimu maisha ya watu 969 kati ya Januari Mosi na Aprili 12 mwaka huu.
Aidha, watu 2,500 wamejeruhiwa katika kipindi hicho, wengine wakisababishiwa ulemavu wa kudumu kutokana na ajali hizo. Hii ina maana kwamba, kwa wastani, watu 10 walipoteza maisha katika ajali za barabarani kila siku kati ya Januari na Aprili 12 mwaka huu, ilhali waliojeruhiwa ni wastani wa watu 25 katika muda kama huo.
Hayo yalibainishwa jana na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Nchini, Mohammed Mpinga aliyesema hayo yametokea katika ajali za barabarani 2,224 za kati ya Januari na mwanzoni mwa Aprili.
Alisema watu 866 walikufa na wengine 2,363 kujeruhiwa kati ya Januari na Machi, wakati wengine 103 wamepoteza maisha na 138 kujeruhiwa kati ya Machi 11 na Aprili 12 mwaka huu.
Alisema katika ajali zote hizi chanzo kikubwa ni mwendokasi wa madereva bila kuzingatia alama na michoro ya barabarani na abiria kushabikia mwendo kasi na kumtetea dereva pindi anapofanya makosa.
“Dereva akifanya makosa akikamatwa abiria wanachangia kumlipia faini dereva jambo ambalo linawapa madereva kiburi wakiamini akifanya makosa abiria wanamsaidia,” alisema Mpinga.
Aliongeza kuwa kwa upande mwingine wamiliki wa vyombo vya usafiri wanachangia ajali kwani wamekuwa wakiwadhibiti na kuwaamrisha madereva wao kwenda mwendo kasi na pale anapokosea anamlipia faini jambo ambalo linapelekea kutokea kwa ajali zinazopoteza maisha ya watu wengi na kuwaachia wengine vilema vya maisha.
Alisema pia tabia binafsi za madereva kuendesha kwa ubabe barabarani pindi wanapokutana na magari madogo, kitendo alichosema si sahihi kisheria na linaweza kusababisha ajali hivyo ni vyema kila mmoja kumheshimu mwenzake na kufuata sheria.
Pia alisema jambo lingine linalosababisha ajali za barabarani ni matumizi ya dawa za kulevya na ulevi mambo ambayo humfanya dereva kuchoka na matokeo yake kusababisha ajali.
Aidha aliwataka madereva kuwa na tahadhari wanapoendesha hususani vipindi vya mvua, akiwahimiza kuwa waangalifu na kuzingatia michoro na alama za barabarani na abiria kutoa taarifa za madereva wanaokwenda kinyume na sheria za barabarani. JK atuma salamu Wakati Mpinga akianika takwimu hizo,
Rais Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Rajabu Rutengwe kuomboleza vifo vya watu 19 na wengine 11 waliojeruhiwa katika ajali ya basi na lori iliyotokea mwishoni mwa wiki katika kijiji cha Msimba kwenye Barabara Kuu ya Morogoro – Mbeya, kilometa chache kutoka Ruaha Mbuyuni na kusababisha abiria hao 18 kuungua vibaya.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, alisema: “Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu 18 kutokana na ajali mbaya ya barabarani iliyosababisha miili yao kuungua vibaya.
“Huu ni msiba mkubwa kwa Taifa, hivyo nakutumia salamu zangu za rambirambi, na kupitia kwako naomba salamu zangu za rambirambi na pole nyingi ziwafikie pia wanafamilia, ndugu na jamaa waliopotelewa na wapendwa wao katika ajali hiyo.
Namuomba Mola awape moyo wa uvumilivu na subira watu wote waliopotelewa na ndugu na jamaa zao katika ajali hiyo mbaya.
Vilevile namuomba Mola awawezeshe majeruhi wote wa ajali hiyo kupona haraka, ili warejee katika hali yao ya kawaida na kuungana tena na familia, ndugu na jamaa zao,” aliongeza kusema Rais Kikwete.