Wednesday, 18 March 2015

KATIBA INAYOPENDEKEZWA NI MWIBA MCHUNGU KWA WAPINZANI NA MAASKOFU WANAOIPINGA.





 Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Vuai Ali Vuai

SIKU moja baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kuonya juu ya waraka wa maaskofu wa kutaka wananchi waikatae Katiba Inayopendekezwa, wanaoisakama Katiba hiyo wamezidi kubanwa na kuonekana wasioitakia mema Tanzania.


Pamoja na kuunga mkono `karipio’ la Kardinali Pengo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM -Zanzibar, Vuai Ali Vuai amesema viongozi wa kambi ya upinzani na washirika wao hawaitaki Katiba Inayopendekezwa kwa sababu wanajua wazi kwamba ndiyo mwarobaini wa ufumbuzi wa kero zote, zikiwemo za Muungano zilizokuwa zikipigiwa kelele na viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) wakiwemo wa upinzani.

Vuai alisema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya wajumbe wa Sekretarieti ya mikoa na wilaya ya CCM kwa ajili ya kupigwa msasa na kujitayarisha kutoa mafunzo ya Katiba Inayopendekezwa kwa wanachama katika shehia mbalimbali, Kendwa, mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema wapinzani wanajua fika kuwa Katiba Inayopendekezwa imezipatia ufumbuzi kero zote za Muungano zilizokuwepo awali kwa hivyo hawana jipya na hilo ni pigo kwao kuelekea katika Uchaguzi Mkuu wa baadaye mwaka huu.

“Wananchi wengi wanawashangaa wapinzani na viongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa sababu wao walipokuwa Baraza la Wawakilishi walikuwa wakilalamika kero za Muungano na kukubaliana kuzipatia ufumbuzi katika Bunge Maalumu la Katiba ambalo mara baada ya kuanza kikao chake walisusia…” alisema.

Alitaja suala la nishati na mafuta ambalo awali lilikuwa katika orodha ya mambo ya Muungano, lakini wajumbe wa Bunge la Katiba walikubaliana na kuipa uwezo Zanzibar sasa kushughulikia rasilimali hiyo wenyewe.

Alisema tayari wawekezaji mbalimbali wameonesha nia ya kuja nchini kuwekeza katika sekta ya nishati pamoja na nchi nyingine kukubali kuwasomesha vijana wa Kitanzania katika sekta hiyo, lakini wapinzani wamekuwa wakiwavunja moyo wananchi kwa kuwashawishi kuikataa Katiba Inayopendekezwa ambayo maslahi yake kwa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla ni makubwa.

Vuai alifafanua na kusema viongozi wa CUF wameonesha udhaifu mkubwa na kasoro katika uongozi wa nchi huku wakiweka mbele maslahi yao binafsi kuliko faida ambayo wananchi wa Zanzibar watapata.

Aliwataka viongozi watakaokwenda kwa wananchi kuichambua Katiba Inayopendekezwa kifungu kwa kifungu zaidi katika vifungu ambavyo vimelenga na kutaja maslahi ya Zanzibar katika mambo ya Muungano.

Alisema CUF katika Katiba Inayopendekezwa walikuwa wakitaka suala moja tu la Muungano wa mkataba na baada ya kukataliwa rai yao hiyo walikuja na Muungano wa Serikali tatu, huku wakikubali kuunganisha nguvu na baadhi ya vyama vya upinzani vilivyozaa umoja unaojulikana kama Ukawa.

Usomaji wa Katiba
Wakati Vuai akifichua kile kinachoonekana kuwa ni siri ya wapinzani na washirika wake kuikataa Katiba Inayopendekezwa, Serikali imesisitiza kuwa, wananchi wanapaswa kuachiwa fursa ya kujiamulia wenyewe juu ya aina ya Katiba wanayoitaka, maamuzi wanayoweza kuyafanya baada ya kusoma kwa kina Katiba Inayopendekezwa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi nakala ya Katiba Inayopendekezwa kwa taasisi na makundi mbalimbali, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Asha-Rose Migiro alisema: “Wananchi wanapaswa wapewe fursa waisome Katiba Inayopendekezwa kisha wachukue maamuzi wao wenyewe bila kushinikizwa na mtu, au kikundi chochote kuhusiana na kupiga kura.”

Akiuzungumzia waraka wa Baraza la Maaskofu (TEC) na Jukwaa la Wakristo uliotolewa na kusomwa sehemu mbalimbali ikiwa pamoja na nyumba za ibada, Dk Migiro alisema amefurahishwa na kauli ya Kardinali Pengo ya kuwaonya viongozi wa dini kutoingilia uhuru wa waumini wao, kwani kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na maadili ya kazi yao.

“Nimefurahishwa sana na kauli ya Kardinali Pengo na kila mtu anapaswa aheshimu kauli hiyo. Pindi muda ukifika wa kupiga kura hapo Aprili 30 mwaka huu, apige kura kwa kujiamulia mwenyewe,” alisema Dk Migiro aliyesisitiza hakuna mabadiliko ya tarehe juu ya siku ya kupiga Kura za Maoni.

Akimkaribisha Dk Migiro kukabidhi nakala za Katiba Inayopendekezwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Maimuna Tarishi alisema jumla ya nakala 658,700 kati ya zaidi ya milioni 2 zinatarajiwa kugawiwa kwa taasisi za kidini, wizara za serikali na mashirika ya umma na yasiyo ya kiserikali.

TEC, CCT wakosolewa
Mmoja wa wasomi na mchambuzi mahiri wa masuala ya siasa nchini, Dk Benson Bana wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amezungumzia tamko la TEC na CCT na kusema halina hekima na limelenga kuligawa taifa.

“Nilipousoma sikuamini kama kweli umetolewa na maaskofu mpaka pale nilipoona saini zao. Inasikitisha kuona maaskofu ambao wana nafasi kubwa katika jamii na ni kimbilio pale panapokuwa na shida kutoa tamko la kuegemea upande mmoja,” alisema.

Alisema si vyema kwa maaskofu kutoa tamko kama hilo katika mazingira ya sasa na kuwa walitakiwa kutafakari kabla ya kutoa waraka huo.

“Labda watuambie kuwa TEC na CCT ni vikundi vya kiraia kwa kuwa na upande, na tamko kama hili linafanya tuhoji taifa linakwenda wapi hasa katika madaraka, yaliyotokea Rwanda na Somalia yalianza watu wenye madaraka ambao wana ushawishi mkubwa katika koo zao na dini zao kuonesha misimamo yao.”

Alisema maaskofu wanatakiwa kujua kuwa mradi wa kujenga taifa kuwa taifa la amani ni endelevu na ulianza mwaka 1961 nchi ilipopata uhuru na bado kuna wajibu kuendelea kujenga amani ya nchi.

“Kama leo wametoa tamko hilo Wakristo na Waislamu nao watoe yao na jumuia nyingine zitoe zao unadhani athari yake itakuwaje?,” alisema na kuhoji maaskofu walikuwa wapi kukosoa Katiba ya 1977 ambayo ina mapungufu. Bana aliongeza: “Suala la wananchi kupigia kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa ni haki ya Watanzania, na sasa maaskofu wasinyang’anye haki hiyo, ya Kaisari wamwachie Kaisari.”.HABARILEO