Musa Mateja/mchanganyiko
MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amepatwa na mshtuko mkubwa baada ya kuwepo madai ya kudaiwa kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 800 na serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Risasi Mchanganyiko linakupa mchapo kamili.
Msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’
ILIKUWAJE?
Mwishoni mwa wiki iliyopita, barua inayodaiwa kuandikwa na mamlaka hiyo halali ya serikali, ilisambazwa mitandaoni, ikielezwa kuwa ilikuwa imetumwa kwa meneja wa msanii huyo ambaye kwa sasa ndiye yupo juu, ikimtaka kupeleka nakala za mikataba yote ya muziki aliyoingia kwa ajili ya kufanya shoo, kuanzia mwaka 2010 hadi sasa.
GUMZO MITANDAONI
Baada ya kuwekwa kwa barua hiyo mitandaoni, watu mbalimbali walitoa maoni yao walionyesha hisia tofauti, baadhi wakipinga kwa madai kuwa wanamuonea huku wengine wakisema siyo Diamond tu, bali wasanii wote wanastahili kulipa kodi kutokana na mapato wanayopata kupitia kazi zao.
KODI ZIPOJE KIBONGOBONGO?
Mtaalam mmoja wa mambo ya kodi aliyezungumza na Risasi Mchanganyiko, alisema kwa mujibu wa taratibu zao, msanii huyo anastahili kulipa kodi kiasi cha asilimia kumi ya fedha anazopata katika kila mkataba anaoingia.
“Kuna walipa kodi wengine kama wafanyabiashara, hawa wanalipa kile ambacho kitaalamu kinajulikana kama Capital Gain, yaani kulipa kadiri unavyopata. Mtu anakwenda TRA mwenyewe na kueleza mapato yake na mamlaka itampangia kiasi cha kulipa. Ila watu kama wasanii na wengine wanaolipwa, wanatakiwa kutoa asilimia kumi ya malipo,” alisema mtaalam huyo aliyekataa kutajwa jina gazetini.
DIAMOND ANADAIWA SH. NGAPI?
Kama suala hilo litafanyika kwa mujibu wa mtaalam huyo, Diamond ambaye malipo yake kwa shoo moja yanatajwa kuwa ni shilingi milioni 20 kwa sasa, atatakiwa kulipa kiasi kinachozidi milioni 800 kutokana na hesabu zilizofanywa na watu wanaofuatilia muziki wake.
“Jamaa anafanya wastani wa shoo kama tatu kwa mwezi hapa nyumbani (Tanzania) na tatu zingine nje. Zile za nje analipwa siyo chini ya dola 25,000 kwa shoo moja. Nadhani unajua kwa sasa huyu dogo ndiye anakimbiza sana katika soko, yupo juu na kila promota anahitaji huduma yake,” alisema mdau huyo wa Bongo Fleva.
MCHANGANUO ULIVYO
Kama hesabu za mdau huyo zitakuwa sawa, inamaanisha kuwa Diamond anaingiza wastani wa shilingi milioni sitini kwa mwezi hapa nyumbani, na milioni 127 kwa mikataba ya nje ya nchi (Dola moja ya Marekani ni sawa na shilingi 1700), ikimaanisha kuwa kwa mwezi mmoja, kijana huyo aliyekulia Tandale, anaingiza kiasi cha shilingi milioni 187.5.
JUMLA YA MAPATO MIAKA MINNE
Kwa mahesabu hayo, Diamond Platnumz anaingiza wastani wa shilingi bilioni 2.2 kwa mwaka, fedha ambayo ukijumlisha kwa miaka minne, ameweka kibindoni shilingi za kitanzania bilioni 8.8, ambazo asilimia kumi yake ni shilingi milioni 880, ambazo ndizo zinazotakiwa kulipwa.
MENEJA AFUNGUKA
Mmoja wa mameneja wa Diamond, Babu Tale alipotafutwa na gazeti hili na kuulizwa kama ni kweli alipewa barua au kujua kuwa barua hiyo ipo, alikataa kulizungumzia suala hilo, akisema siyo jambo la kulielezea kwenye vyombo vya habari.“Hata mimi nimeiona hiyo barua (anautaja mtandao wa kijamii maarufu sana nchini), sina cha kuelezea kwenye media,” alisema meneja huyo huku akikataa katakata kusema kama ameipata au la.
DIAMOND MWENYEWE SASA
Baadaye Risasi Mchanganyiko liliwasiliana moja kwa moja na Diamond mwenyewe, ambaye alikuwa nchini Nigeria, alikoenda kwa ajili ya shoo iliyoandaliwa na Africa Magic Viewers Choice Awards jijini Lagos, alishtuka sana na kuomba asizungumzie suala hilo.“Daah! Milioni 800? Anyway naomba nisizungumzie suala hilo kwa sasa.”
TRA WAIKANA BARUA
Gazeti hili lilipomtafuta ofisa wa TRA, ambaye jina lake limeandikwa katika barua hiyo, aitwaye Tillya V.M. T, alikanusha kuandika barua hiyo na kusema ni mambo ya kugushi yanayofanywa mitandaoni.
“Hakuna kitu kama hicho, its something created,” alisema bosi huyo akimaanisha kuwa jambo hilo ni la kutengenezwa.
NYOTA YA WEMA YAHUSISHWA Wakati hayo yakijiri, baadhi ya wadau wamesema suala hilo linahusishwa na mojawapo ya kauli iliyowahi kusemwa na aliyekuwa mpenzi wake, Wema Sepetu kuwa mwanaume yeyote anayekuwa naye kwenye uhusiano wa kimapenzi, nyota yake hung’aa, lakini anapoachana naye, hufifia.
WENGINE WAMHUSISHA ZARI
Aidha, wadau wengine walisema ishu hiyo huenda imeibuka kama mkosi uliochangiwa na kujiingiza katika mapenzi na mwanadada raia wa Uganda, Zarina Hassan ‘Zari’ ambaye mashabiki wanadai ni mtu mwenye mikosi, kwani Diamond ni mwanaume wake wa nne rasmi, wa tatu wa kwanza kila mmoja akiwa amezaa naye.
Source: GPL