Wanafunzi wawili wanaosoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wameumia baada
ya moto kuteketeza hosteli za Mabibo Dar es Salaam, walikokuwa wakiishi.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tukio hilo, Makamu Mkuu wa
Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala, alisema moto huo
uliteketeza ghorofa ya tatu ya jengo A linalotumiwa na wanafunzi wa kike.
“Tunamshukuru Mungu hakuna maafa yaliyotokea ingawa kuna wanafunzi
wawili wamepata matatizo na tayari tumeshawakimbiza Hospitali ya Taifa
Muhimbili kwa matibabu.
“Mmoja alijirusha kutoka ghorofa ya tatu kuokoa maisha yake baada ya
kuona hakuwa na njia mbadala na mwingine alipoteza fahamu ghafla baada ya moto
kuanza kuwaka katika jengo alimokuwa akiishi.
“Kwa hiyo kwa sasa tunafanya utaratibu wa kuangalia jinsi
tutakavyowasaidia wanafunzi waliopatwa na matatizo ya kupotelewa na vifaa na
nasema chuo kitahakikisha wanapatiwa huduma zote muhimu,” alisema Profesa
Mukandala.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Polisi wa Kinondoni, Camillus Wambura, alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo, ulinzi uliimarishwa kudhibiti wizi na uharibifu mwingine ambao ungefanywa na watu
wasiokuwa waaminifu.
“Taarifa ninazo na tayari ulinzi tumeshauweka kwa kushirikiana na polisi
jamii.
“Pamoja na hayo, nawashauri wanafunzi wote waliopoteza mali zao waende
kituo cha polisi kutoa taarifa na ikiwezekana wapatiwe msaada wowote
watakaouhitaji.
“Nasema hivyo kwa sababu wakati wa uokoaji, baadhi ya mali zilikuwa
zinatupwa nje kupitia madirishani na hali hiyo ilisababisha baadhi yake kupotea
ila vinaweza kupatikana kwa msaada wa polisi,” alisema Kamanda Wambura.
Kutokana na hali hiyo, alisema Jeshi la Polisi litaendelea kuweka
ulinzi eneo la tukio hadi uongozi wa chuo utakapowapatia wanafunzi wote maeneo
mengine salama ya kuishi.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Ubungo Kibangu zilipo hosteli hizo,
Deusderi Ishengoma, alisema madhara yaliyotokea yangekuwa makubwa kama moto huo
ungewaka usiku.
“Kama unakumbuka siku za nyuma wanafunzi hawa walishaandamana
kuilalamikia TANESCO kwamba inashindwa kuimarisha mfumo wa umeme katika hosteli
hizo na kusababisha ukatikekatike mara kwa mara.
“Kwa hiyo inawezekana yale malalamiko ndiyo yamesababisha madhara kwa
sababu inaonekana tatizo halijatatuliwa,” alisema Ishengoma.