Saturday, 16 May 2015

Siwema wa Nay wa Mitego Yazidi Kumkuta..Apandishwa Kizimbani Kwa Kosa la Kujipatia Mali na Pesa Kwa Vitisho

MAJANGA yamezidi kumkuta mzazi mwenzake na Mbongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’, Siwema Edson ambapo jana alitarajiwa kufikishwa  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, kujibu shitaka la kujipatia mali kwa njia vitisho.
Siwema anatuhumiwa kujipatia mali kwa kumtishia kigogo mmoja serikalini (jina tunalihifadhi) ambaye inadaiwa alikuwa mchumba wake na baada ya kuachana, mrembo huyo kwa nyakati tofauti akawa anamtishia kuwa ana picha zake za utupu hivyo asipompa fedha ataziweka mitandaoni hivyo kigogo huyo alikuwa akilazimika kumpatia.

Chanzo cha habari hii kimeeleza kwamba, baada  ya polisi kujiridhisha na uchunguzi wa madai hayo, waliamua kumpeleka mahakamani ili kujibu shitaka hilo linalomkabili.

“Kesho (jana) wanampandisha mahakamani akajibu shitaka linalomkabili maana polisi tayari wameshamaliza uchunguzi wao hivyo sakata hilo linahamia mahakamani,” kilisema chanzo chetu.

 Alipotafutwa Siwema kwa njia ya simu, simu yake iliita bila majibu lakini alipopigiwa msaidizi wake wa dukani aitwaye Zuhura, alisema:

“Dada (Siwema) jana alikuwa polisi hivyo sijajua kama wamempeleka mahakamani au la!”

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna wa Polisi, Charles Mkumbo alikiri kumkamata Siwema kwa kosa la kujipatia mali kwa njia ya vitisho kisha kumuachia kwa dhamana.