Chama cha Alliance for
Change and Transparency (ACT), kimesema kinatarajia kunyakuwa majimbo manne ya
ubunge katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba, mwaka huu.
Kimetaja majimbo hayo
kuwa ni Ubungo, ambalo linaongozwa na John Mnyika (Chadema), Kawe
linaloshikiliwa na Halima Mdee (Chadema), Segerea ambalo Mbunge wake ni
Makongoro Mahanga (CCM) na Kahama la James Lembeli (CCM).
Kiongozi Mkuu wa
Chama hicho, Zitto Kabwe, alisema hayo katika kipindi cha Hot Mix kinachorushwa
na kituo cha EATV.
Zitto aliendeleza
msimamo wake wa kutogombea ubunge kwenye jimbo lake la awali la Kigoma
Kaskazini.
“Nina maombi jimbo la
Kahama, Kawe, Ubungo na Segerea lakini kwa kuwa ACT kinaongozwa kizalendo,
tutaweka utaratibu mzuri wa kuweka wagombea kila eneo, binafsi kwa sasa siwezi
kusema wapi nitagombea,” alisema.
Alipoulizwa ni eneo gani
kati ya hayo aliyoyataja huduma yake inahitajika, alijibu kwa kifupi kuwa, nchi
nzima ina muhitaji.
“Kabla ya kampeni
kuanza wagombea wakirudisha fomu ndipo mtajua Zitto anagombea jimbo gani,
lakini lazima niongozwe na chama nikagombee wapi , wanaweza kusema Zitto
kagombee jimbo A,” alisema.
Aliongeza kuwa, ACT
kinahitaji kujipanga kuingia kwenye mapambano ya kufyeka msitu wa siasa kwa
kuwa ndani yake kuna vyama zaidi 22 na vingine vikiwa na uzoefu mkubwa kutokana
na kudumu zaidi ya miaka 23.
Alisema kazi kubwa
walionayo ni kukijenga chama ili kiweze kulirudisha taifa kwenye misingi ya
waasisi waliyoiacha.
Aliongeza kuwa, baadhi
ya watu wanamuona kama anaanza upya kwa sababu wapo wachache waliwahi kujaribu
na kuishia njiani.
Alipoulizwa kuhusu
wachambuzi wa siasa wanavyomchukulia hivi sasa, Zitto alisema wapo wenye
mtazamo hasi na wengine chanya.
Alisema kwa wale
wanaomchukulia kwa mtazamo hasi anaendelea kuwafundisha na kuwaonyesha
kwamba muono wao ni tofauti wakati wale wa chanya anaendelea kuwasikiliza ili
kupata muongozo zaidi kutoka kwao.
“Tukumbuke hii nchi
watu wamezoea kuchukia mabadiliko angalia kwenye sanaa wakimuona Diamond
amefanikiwa waanza kutoa maneno ambayo siyo, watu wanachukia mabadiliko,”
alisema.