Saturday 21 March 2015

Kikwete: Wanachama wa EAC wamalize tofauti zao



Rais Jakaya Kikwete wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC, amezitaka nchi wanachama wa jumuiya hiyo kupuuza tofauti zao na kuongeza ushirikiano zaidi katika uwanja wa kimaendeleo kama njia ya kuendeleza jumuiya hiyo.


Rais Kikwete aliyasema hayo wakati alipokuwa akihutubia Bunge la Afrika Mashariki mwanzoni mwa kikao cha Bunge hilo, jijini Bujumbura nchini Burundi ambapo aliashiria pia hali halisi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki hivi sasa.



Alisisitiza kuwa, hali ya baadaye ya EAC inategemea ni jinsi gani wananchi wa nchi wanachama wanavyohisi kunufaika na kuwepo kwa jumuiya hiyo na uanachama wa nchi zao. Aidha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amewataka wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki kujishughulisha na mambo yatakayoiletea faida jumuiya hiyo, badala ya kila mbunge kujikita katika kushughulikia mambo yatakayoliletea faida taifa lake.