Friday 20 March 2015

RATIBA LIGI KUU TANZANIA BARA, SIMBA ,YANGA, AZAM NYASI ZITACHIMBIKA.






Ligi kuu Tanzania bara kuendelea kesho kwa mechi mbili kupigwa miji miwili nchini.

Maafande wa jeshi la kujenga Taifa, Mgambo JKT wataikaribisha Dar Young Africans katika uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga.



Mgambo walioifunga Simba jumatano ya wiki hii mabao 2-0 watakutana na Yanga iliyofungwa 2-1 katika uwanja huo msimu uliopita. Tayari Yanga ipo jijini Tanga toka jana na asubuhi hii wamefanya mazoezi uwanja wa Mkwakwani.

Kocha msaidizi wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa 'Master' amesema: "Tutakabiliana na Mgambo ambao ni wagumu kufungwa Mkwakwani, lakini kila jambo lina mwisho wake".
Kocha Mkuu wa yanga nae amesema : "Najua kwamba tunakwenda kucheza mchezo katika uwanja mgumu ambao sasa naujua vyema na tutumie mbinu gani katika kupata ushindi, furaha yangu ni kwamba nitakuwa na wachezaji wangu wote ambao hawakuwepo katika mechi zilizopita.”

 


Nae Kocha wa Mgambo Hakusita kuwakumbusha wana Yanga kile kilichowakuta Simba na Yanga kwa msimu uliopita, 
“Unajua labda mimi niwe tofauti kidogo naweza kusema nimewafunga Simba kwa kutumia taarifa za magazeti juu ya maandalizi yao, Simba wasiwe na sababu nyingi za kusingizia viwanja, mbona wachezaji wao wanacheza mechi za mchangani zenye viwanja kama hiki, watulie tu tulijipanga.”

“Yanga hawatakiwi kuwacheka Simba nao tunawaandalia dozi yao kwa stahiki yao, haya maandalizi tuliyafanya maalumu kwa Simba na sasa tunawageukia wao wanakumbuka niliwafunga tena nikiwa na vijana pungufu.”
Mechi nyingine itashuhudiwa uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara ambapo wenyeji Ndanda fc watachuana na maafande wa JKT Ruvu Stars.

Kocha wa Ndanda fc, Meja mstaafu Abdul Mingange amesema baada ya kufungwa na Azam fc 1-0 mwanzoni mwa wiki hii, lazima JKT wakae kesho.

Ligi hiyo itendelea jumapili ambapo Simba SC watakuwa wageni wa Ruvu Shootings uwanja wa Taifa Dar es salaam.

Tanzania Prisons watachuana na Polisi Morogoro uwanja wa CCM Sokoine Mbeya.
Kibarua kingine kikali kitakuwa uwanja wa CCM Mkwakwani Tanga, Coastal wakiwakaribisha Azam fc.