Ndugu Waandishi wa habari, wanachama na wapenzi wa ACT-Wazalendo na
wote mliohudhuria mkutano huu, Kama mnavyojua siku ya Ijumaa tarehe 19 Machi 2015 ilikuwa siku yangu
ya mwisho kuhudhuria bunge la kumi linaloendelea Mjini Dodoma. Baada ya kung’atuka ubunge kufuatia kukoma uanachama wangu wa chama
nilichotumia kuingia Bungeni, wengi mliniuliza ‘what is next?’
Sasa ninapenda kuwataarifu, kama ambavyo baadhi yenu tayari mnajua,
kwamba jana siku ya Jumamosi tarehe 20 Machi 2015 nilijiunga rasmi na Chama cha
ACT - Wazalendo na kukabidhiwa kadi na Mwenyekti wa Tawi la Tegeta. Hii ilikuwa
ni moja kati ya siku muhimu kabisa katika maisha yangu ya kisiasa. Na kwa leo
kwa kweli nisingependa nizungumzie mgogoro uliokuwepo kati yangu na viongozi
wangu wa chama cha zamani wala kile kilichotokea Bungeni. Hayo yote mnayajua,
yameandikwa sana na yameshapita. Sasa ni wakati wa kusonga mbele. Rais Kwame
Nkrumah alipata kusema "forward ever, backward never". Na kama
nilivyosema Bungeni, yaliyopita si ndwele, tugange yajayo. Kwa hiyo leo
nitazungumzia uanachama wangu katika chama changu kipya cha ACT - Wazalendo.
Tuna vyama 22 kwa sasa. Na kwa kweli wengi watakuwa wanajiuliza kwa
nini nijiunge na chama kipya ambacho kimeanzishwa juzi tu na ambacho pengine
wanachama wake bado wanajaa katika kiganja cha mkono?
Nimejiunga na ACT kwa sababu ninaona kwamba huku ndiko kunakoendana na
kile ambacho mimi nimekipigania kwa miaka yote tangu nianze siasa, ambacho ni
kuweka mbele maslahi ya Taifa dhidi ya kitu kingine chochote. Kwa kifupi
nimepigania uzalendo kwa nchi yangu na huu ndiyo msingi mama wa Chama cha ACT -
Wazalendo.
Kama mnavyojua mimi ni mjamaa na ninaamini katika misingi ambayo
Mwalimu Nyerere aliisimamia. ACT-Wazalendo ni chama pekee nchini
kinachokubaliana na Itikadi ya ujamaa na kinaamini katika Falsafa ya Unyerere
ikiwa na lengo la kuirudisha nchi katika misingi iliyoasisi taifa. Ninajiunga
na ACT-Wazalendo kwa sababu ni chama kinachoamini katika msingi wa uadilifu na
kimeweka miiko na maadili ya viongozi katika kuhakikisha kwamba viongozi wote wa
ACT-Wazalendo wanakubaliana nayo kwa kusaini. Naamini kuwa na miiko na maadili
kwa viongozi ni mwanzo wa kuhakikisha kwamba jamii yetu inaishi katika uadilifu
na kwamba viongozi wanakuwa mfano wa uadilifu katika jamii.
Uadilifu ni nguzo
muhimu katika kujenga mfumo madhubuti wa uwajibikaji nchini kwetu. Mtakumbuka kwamba katika miaka yangu yote ya ubunge nimepigania
uwajibikaji na uwazi. Hii ni misingi ambayo ninaamini kwamba ni moyo wa
utumishi wa umma. Nimefurahi kwamba kati ya misingi kumi ya ACT-Wazalendo,
uwajibikaji na uwazi ni sehemu muhimu kabisa ya misingi hiyo. Uwazi ni sehemu
ya jina la chama hiki. Yote haya yamenifanya nione kwamba sitojiona mgeni
katika chama hiki. Huku ndiko nyumbani kwangu kisiasa na katika utumishi wa
umma.
Nimejiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu ninakubaliana na imani yao
kwamba Kujitegemea, bidii, umakini na weledi katika kazi ndiyo msingi wa
maendeleo. Hakuna namna nchi yetu na wananchi watapiga hatua ya kimaendeleo
bila sisi sote kufanya kazi kwa bidii na kwa kuzingatia umakini na weledi.
Ninakubaliana na ACT-Wazalendo kwamba raslimali za Taifa lazima zitumike
kuondosha umaskini wa watu wetu. Ninajiunga na ACT-Wazalendo kwa sababu
ninakubaliana na imani yao kwamba Umoja ni ngao muhimu katika ujenzi wa taifa
letu na Afrika kwa ujumla. Lazima tuirudishe nchi yetu katika misingi
iliyoasisi taifa hili. Lazima tuirudishe nchi yetu katika heshima na uongozi wa
bara hili la Afrika.
Ninaahidi kufanya kazi na vijana, wanawake, wanaume na watu wote
wanaoamini katika siasa safi na siasa za hoja. Tunataka tufungue ukurasa mpya
wa siasa hapa nchini. Siasa za masuala ya nchi yetu. Siasa za masuala ya
vijana, wanawake, wazee, wakulima, wafanyakazi, wajasirialimali,
wafanyabiashara na wote wanahangaika kuijenga nchi yetu na katika kuondoa umaskini.
Tunataka tuzungumze namna bora ya kuendesha elimu, afya, hifadhi ya jamii, na
ajira. Tunataka tujenga hoja mbadala kuhusu namna endelevu ya kujenga uchumi
shirikishi ambapo kila mwananchi anajisikia sehemu yake.
Mwezi Oktoba mwaka 1966 Mwalimu Nyerere alipokea maandamano ya
wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Ikulu. Maandamano yale yalichochewa
na kasi kubwa ya rushwa na maisha ya kifahari ya viongozi (wabenzi). Mwalimu
alifoka kwa kuuliza “ Tunajenga nchi ya namna gani”? Hatimaye Azimio la Arusha
likatangazwa.
Chama hiki kipya kimeanzishwa katika mazingira yale yale ya mwaka 1966.
Ni wakati wa kujiuliza na kupata majawabu ya aina ya nchi tunayojenga. Sisi ACT
– Wazalendo tumeona jawabu ni kurudi kwenye misingi. Waingereza wanasema ‘back
to the future’ Let the new beginning begin.