WAZIRI wa Kazi na Ajira Mhe. Gaudensia
Kabaka (pichani) amesoma Muswada wa Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini
wa mwaka 2014 kwa mara ya pili ikiwa muswada huu umelenga masuala mbalimbali
ikiwemo mabadiliko ya kiuchumi pamoja na mahitaji ya kiteknolojia ambayo ni
kichocheo kikubwa cha uhamiaji wa nguvu kazi kutoka nchi moja kwenda
nyingine.
Mhe.Kabaka alisema kwa sasa zipo
mamlaka nyingi zinzotoa vibali vya ajira kwa wageni kwa kuzingatia sheria
zinazosimamia maswala ya Uhamiaji, Uwekezaji, Elimu, Biashara na Wakimbizi,
hivyo hali hii ya kuwepo na mamlaka nyingi zinachangia kusababisha
usumbufu kwa wawekezaji na kokosekana kwa uwajibikaji pamoja na kuwepo na
udanganyifu.
“Kutungwa kwa sheria hii kunalenga
kutelekeza kwa manufaa ya nchi yetu mikataba ya kikanda inayoruhusu uhamiaji
huru wa nguvu kazi hususani inayohusu itifaki ya soko la pamoja la Jumuiya ya
Afika Mashariki na Ushirikiano wa Jumuiya ya nchi za kusini mwa Afrika SADC”
alisema Mhe. Kabaka.
Katika kutekeleza mikataba ya kikanda na
kimataifa kuhusu uhamiaji na nguvu kazi, utaratibu wa kutoa vibali vya ajira
kwa wageni umekuwa ukitumika ili kuhakikisha nguvu kazi ya wageni hao inaleta
manufaa kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na pia katika kulinda ajira za
wananchi.
Kwa upande wa Msemaji Mkuu wa kambi
rasmi ya upinzani Mhe.Celina Paresso Mbuge wa Viti Maalum-CHADEMA aliishauri
Wizara ya Kazi na Ajira kushirikiana na wizara mtambuka kama Wizara ya Viwanda
na Biashara na Idara ya Uhamiaji, kufanya ukaguzi wa vibali vya ajira hasa
katika maeneo ambayo raia wa kigeni wanafanya shughuri zao bila kuzingatia
sheria za nchi.
“Tanzania tuna maliasili nyingi, lakini
dunia ya leo na ijayo itatawaliwa na wenye maarifa, kwa maana ya sayansi,
teknolojia, elimu na ujuzi” alisema Mhe. Paresso
“kuwa na maliasili peke yake haitoshi,
hatuna budi tujinoe kwa elimu na ujuzi, na hasa elimu inayomuwezesha mtu
aajirike au ajiajiri” aliongezea Mhe. Paresso
Endapo Mhe. Rais ataridhia, Sheria hii
itaanza kutumika tarehe 1 Julai, 2015. Kutungwa na kuanza kutumika kwa Sheria
ya Ajira ya Wageni Nchini kutakuwa na matokea chanya ikiwema uratibu mzuri wa
ajira za wageni nchini, kuongezeka kwa ajira za watanzania na kuongezeka kwa
ujuzi kwa wafanyakazi wa Tanzania.